YANGA WAJA NA MPANGO WA KUSAJILI MSHAMBULIAJI KUTOKA BENIN
Uongozi wa Klabu ya Yanga wanafanya mazungumzo na straika kutoka Benin, Marcelin Koukpo na kama wakimalizana naye, Ngoma anaweza kufungasha mabegi yake na kama atabakia anaweza kuwa mtokea benchi.
Straika huyo ni yule aliyeisumbua ngome ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars,’ katika mchezo wa kirafiki wa Kimataifa, uliochezwa nchini humo na kumalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.
Taarifa za uhakika kutoka Yanga zinadai kuwa, kigogo mmoja amekuwa akifanya mazungumzo na straika huyo na siku yoyote wanaweza wakamalizana na kama itakuwa hivyo, mabingwa hao watetezi watakuwa wamelamba dume.
Hicho ndicho kinachowachelewesha Yanga kufanya maamuzi ya kumwadhibu Ngoma, kutokana na utovu wake wa nidhamu, kwani wanasubiri dili hilo litiki ndipo wachukue maamuzi magumu kwa Mzimbabwe huyo.
Ngoma amekuwa kama adui mkubwa wa Yanga kutokana na tabia zake zinazodaiwa za kujiona yeye ni mkubwa kuliko timu hiyo, kitu ambacho kinawafanya hata mashabiki kutamani aondoke zake, kwani wapo wachezaji waliokuwa na viwango zaidi yake walioondoka na timu ikaendelea kuwapo.
Mzimbabwe huyo aliondoka kwenda kwao bila ruhusa ya uongozi, na aliporejea aliambiwa aandike barua ya kujieleza (utetezi) na sasa anasubiri maamuzi ya uongozi kujua kama atasamehewa ama la.
Taarifa za uhakika kutoka Yanga, zinadai kuwa kama watafanikiwa kuinasa saini ya straika huyo fundi wa kufunga mabao, wanaweza wakavunja mkataba wa Ngoma, baada ya kuchoshwa na usumbufu wake.
Taarifa nyingine zinadai kuwa, hata Amis Tambwe yupo kwenye mstari mwekundu kutokana na umri kumtupa mkono na majeraha ya muda mrefu aliyonayo, lakini kinachoweza kumbakisha ni utulivu na nidhamu aliyonayo Mrundi huyo.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: