WABUNGE TISA WA UKAWA WATAJWA KUHAMIA CCM

Joto la wanasiasa wa upinzani, hasa kutoka vyama vilivyounda Ukawa, kuhamia CCM likiendelea kuongezeka, majina ya baadhi ya wabunge yamekuwa yakihusishwa na wimbi hilo.

Lakini walipotafutwa na Mwananchi, baadhi hawakuwa tayari kutoa msimamo wao kuhusu uvumi huo, wengine walisema watatoa taarifa rasmi leo na baadhi yao walikanusha vikali.

Kwa kauli ya “kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli”, madiwani walianzisha joto hilo kwa kujivua nyadhifa zao na kutangaza kuhamia CCM, lakini Lazaro Nyalandu alibadilisha upepo alipojivua ubunge na kukihama chama hicho tawala, akisema anaungana na wapinzani kupigania Katiba, haki za binadamu na demokrasia.

Sasa wimbi hilo limehamia kwa wabunge baada ya Maulid Mtulia kujivua uanachama wa CUF na ubunge wa Kinondoni mwishoni mwa wiki. Uamuzi wake umefuatiwa na ubashiri kuwa kuna wabunge wengine kadhaa walio safarini.

Habari hizo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii, zikiwakariri baadhi ya wabunge wakiwatuliza wanachama na wafuasi wao wasishangae watakaposikia wenzao wametangaza kuhama upinzani.

Taarifa hizo zinawataja baadhi ya wabunge kutoka Chadema na CUF kwamba wako kwenye mazungumzo ya kuhitimisha safari yao ya kuhamia CCM kwa madai ya “kuunga mkono jitihada za kuleta maendeleo nchini zinazofanywa na Rais Magufuli”.

Baadhi ya wabunge wa Chadema ambao wanatajwa ni Saed Kubenea (Ubungo), James Millya (Simanjiro), Anthony Komu (Moshi Vijijini), John Mnyika (Kibamba), Japhary Michael (Moshi Mjini) na Cecil Mwambe wa Ndanda.

Kwa upande wa CUF ni Zubery Kuchauka (Liwale), Magdalena Sakaya (Kaliua) na Maftaha Nachuma wa Mtwara Mjini.

Taarifa za wabunge hao kuhama zilichagizwa na kauli ya mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliyeandika katika akaunti yake ya Twitter kwamba leo (Jumatano) au Ijumaa kuna wabunge wa upinzani watatangaza kuhama.

Lema alibashiri kuwa mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila aliyekuwa NCCR-Mageuzi na baadaye Chadema, angehamia CCM, akimuelezea kama “mwanasiasa kijana aliyekuwa machachari 2010-2015”.

Katika ujumbe wa juzi, Lema, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliandika: “Kati ya Jumatano (leo) wiki hii na Ijumaa, pesa itakuwa na thamani kwa maisha ya mvulana mmoja ambaye ni mbunge kutoka Chadema.”

Kauli hiyo ya Lema iliamsha mjadala huku anayezungumzwa zaidi kuhama akiwa ni Kubenea ambaye inaelezwa kwamba atahamia CCM, lakini alipoulizwa jana hakuweka bayana.

“Siwezi kuzungumza na chombo kimoja kimoja cha habari. Kesho au keshokutwa nitazungumza. Nipo katika maandalizi na nitaeleza hicho kinachoelezwa,” alisema Kubenea.

Jibu kama hilo lilitolewa na Ole Millya, ambaye alihamia Chadema 2015 wakati wa ‘mafuriko’ ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa.

“Kwa sasa nisijibu chochote, wakati ni dawa,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu hali ya sintofahamu kwa wananchi waliomchagua, alijibu: “Wananchi wangu, najua jinsi ya kudeal nao mimi.”

Baadaye Ole Millya alisema heshima aliyopewa na wana Simanjiro ni kubwa na anatambua hilo, hivyo wapuuze yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii.

Alisema ana njozi ya Simanjiro mpya na aliweka msimamo asizungumze chochote hadi Ijumaa, ila kwa heshima ya wana Simanjiro ameamua kukanusha hilo.

“Nimesema niwajulishe kwa sababu ninyi ndiyo marafiki, mabosi wangu. Nami nataka muwe na ukweli kutoka kwa mbunge wenu. Wacha wapige ramli, waendelee kupiga ramli zao,” alisema Ole Millya.

Kauli ya Ole Millya inalingana na ya Kuchauka ambaye alisema akiwa upinzani anaweza kuisimamia Serikali vilivyo kuliko akiwa CCM.

“Kwanza hawawezi kuja na wakija, unatakiwa uwe umeonyesha mwelekeo huo na mimi ninaamini nikiwa upinzani naweza kuisimamia Serikali na kuisema ila ukiwa CCM unafungwa mdomo na huwezi kuisimamia au kuikosoa,” alisema Kuchauka.

Kauli kama hiyo ilitolewa na Sakaya. “Hao wanaonitaja ni propaganda tu. Mimi ni mtu wa misimamo na sijawahi kuyumbishwa na wala sitegemei kushikiwa akili,” alisema kaimu katibu mkuu huyo wa CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba.

“Mimi ni mbunge, nimekuwa napongeza inapobidi na kukosoa inaponilazimu. Hao wanaoondoka kuwa wanamuunga mkono Rais sijui wamekwenda shule? Kwani ukiwa upinzani huwezi? Wananchi wamekuamini halafu. Nafikiri kuna ajenda na yawezekana wananunuliwa kwa fedha nyingi ambazo mimi siwezi kukubali.”

Mnyika alipotafutwa na Mwananchi alijibu kwa kifupi tu; “sio kweli, ni habari za uongo.”

Hali haikuwa rahisi kwa Mwananchi kumpata Komu, Mwambe na Jafary.

Lakini juzi, meya wa Ubungo Boniface Jacob aliandika ujumbe katika akaunti yake ya Instagram kuwahakikishia wanachama na wafuasi kuwa kuna jaribio la kumng’oa Mnyika.

“Mwambieni... aache kupiga simu ovyo. Tumemrekodi na tutaendelea kumrekodi tumuaibishee. Any time atume sms au apige tena aone,” ameandika katika akaunti hiyo na kuonya kuwa Mnyika si mtu wa kuahidiwa cheo na madaraka ya kuhongwa.

Akizungumza na Mwananchi jana, Meya Jacob alisema walikuwa wakimsumbua Mnyika.

“Niliamua kutoa ufafanuzi huo kwa kuwa tulikuwa na Mnyika halafu wanampigiapigia simu hao (anawataja majina). Ndio maana nikaamua kuandika hivyo kuwa Mnyika hawezi kuhama na kesho (leo) tutakuwa na Kamati Kuu,” alisema.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.