RAIS MAGUFULI AWTEGA WASAIDIZI WAKE

Rais John Magufuli amerejesha fomu inayoonyesha mali na rasilimali alizonazo, huku akimtaka Kamishna wa Maadili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Harold Nsekela kutopokea fomu ya kiongozi yeyote atakayekuwa hajawasilisha tamko lake ifikapo Desemba 31.

“Ikifika Desemba 31 ambayo ni siku ya mwisho kwa mujibu wa sheria, weka mstari na usipokee fomu nyingine. Halafu tuone sheria itafanyaje, nakutakia kazi njema,” alisema Rais Magufuli.

Kauli ya kiongozi huyo mkuu wa nchi huenda ikawaweka kikaangoni viongozi watakaoshindwa kuwasilisha fomu zao ikizingatiwa kuwa leo ni siku ya mwisho ya kazi, huku kesho na keshokutwa zikiwa siku za mapumziko. Dk Magufuli aliwasilisha fomu ya taarifa za mali na madeni yake jana katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasilisha fomu hiyo, aliipongeza Sekretarieti hiyo kwa kazi inazofanya na kutoa agizo hilo kwa Jaji Nsekela.

Naye Jaji Nsekela alimpongeza Rais kwa kutekeleza matakwa ya kisheria yanayomlazimisha kujaza fomu hizo na kusisitiza kuwa ujazaji wa fomu hizo kwa viongozi wa umma si ombi. “Viongozi hawaombwi kujaza fomu hizi. Kuna baadhi wanadhani labda kutuletea hilo tamko ni fadhila, hapana. Sheria ya nchi inahitaji hivyo na kuna sababu zake za msingi,” alisema.

Alisema Rais Magufuli pia amewasilisha taarifa ya akaunti yake ya benki sambamba na tamko hilo, kitendo alichoeleza kuwa ni mfano wa kuigwa na viongozi wengine.

Tamko la viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni linatolewa kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha Sheria namba 13 ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995.

Juzi, Jaji Nsekela alizungumzia urejeshaji wa fomu hizo na kubainisha kuwa kifungu cha 9(1)(b) cha sheria hiyo kinamtaka kiongozi wa umma kupeleka tamko la maandishi linaloorodhesha mali au rasilimali zake, za mwenza wake na za watoto wasiozidi kumi ambao hawajaoa au kuolewa.

Alisema viongozi wapya wanaochaguliwa au kuteuliwa wanatakiwa kujaza fomu hizo na kuzirejesha kwa kamishna wa maadili ndani ya siku 30 baada ya kupewa wadhifa, huku akibainisha hali ya maadili ya viongozi hao hivi sasa ni ya kuridhisha.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.