MTOTO AFARIKI DUNIA AKIVUKA MFEREJI
Mwili wa mtoto anayekadiriwa kuwa na miaka sita umeokotwa katika bwawa la Nabwada lililopo Kata ya Vigaeni mjini Mtwara baada ya kusombwa na maji ya mvua.
Mtoto huyo inaelezwa alisombwa na maji jana Jumamosi Desemba 9,2017 alipokuwa akivuka mfereji. Mwili wake umeopolewa leo Jumapili Desemba 10,2017.
Polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya imetembelea maeneo yaliyoathiriwa na mvua iliyonyesha kuanzia usiku wa kuamkia jana.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda amesema baadhi ya athari za mvua zinatokana na baadhi ya watu kujenga kuta katika mikondo ya maji.
Amesema wamefikia uamuzi wa kuvunja kuta kuanzia kesho ili kuwezesha maji kwenda baharini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ameagiza kuwekwa mipaka katika bwawa hilo ili watu wasiingie kwa usalama wao.
"Watu wasijenge kuingia eneo la bwawa na wale waliojenga ikilazimika tutabomoa kwa usalama," amesema.
Kuhusu tathmini ya athari zilizosababishwa na mvua, amesema bado kamati ya ulinzi na usalama inaendelea na kazi.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: