HUYU NDIYO STRAIKA ANAYEWEZA KUTUA MSIMBAZI MUDA WOWOTE

UNAWEZA kusema vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wamemalizana na straika mpya matata, Jonas Sakuwaha, aliyewahi kukipiga katika kikosi cha mabingwa wa Kombe la Shirikisho barani Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Hatua hiyo inakuja baada ya benchi la ufundi kuridhishwa na uwezo wa straika huyo kwenye mechi yake ya kwanza ya majaribio, Simba wakicheza dhidi ya KMC, Uwanja wa Chamazi.

Katika mchezo huo wa kirafiki uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Sakuwaha alifanikiwa kufunga bao moja Simba wakishinda 3-1, lakini gumzo ikiwa ni umahiri wake ndani ya uwanja.

Straika huyo alionekana kutengeneza muunganiko mzuri kati yake na nahodha John Bocco, ambapo kila alipokuwa akigusa mpira mashabiki wa Simba, walilipuka kwa shangwe, hiyo ikimaanisha kuwa, wameikubali kazi yake.

Baada ya mchezo huo kumalizika, kocha msaidizi wa kikosi hicho, Masudi Djuma, alisema kuwa, kwa upande wao, benchi la ufundi hawana kipangamizi na mshambuliaji huyo, kwani mechi yake ya kwanza tu kaonyesha kwamba ni mmoja wa washambuliaji wenye uwezo mkubwa.

“Binafsi huyu mchezaji namjua vema namna anavyotimiza majukumu yake, unaona mechi yake ya kwanza tu alichokifanya, hapo ametoka kwenye mapumziko, hajafanya mazoezi ya kutosha, niseme kilichobaki ni kwa upande wa viongozi kuangalia namna ya kumpa mkataba.

“Siwezi kusema moja kwa moja tunamsajili kwa kuwa kuna upande wa viongozi, wanakuwa jukwaani wanaangalia, ndiyo maana ya mechi hizi za kirafiki, lakini pia masuala ya mikataba yana mapana yake kwa pande zote mbili,” alisema.

Mbali na straika huyo kuichezea TP Mazembe, pia amewahi kuitumikia klabu nyingine mbili kubwa Afrika, ikiwamo Zeco United ya kwao Zambia na El-Mereikh ya Sudan.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.