MTU MMOJA AFARIKI DUNIA KWA KUNYWA GONGO MKOANI RUKWA

Kijana mmoja katika kijiji cha Myenge kata ya Kirando wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, aliyejulikana kwa jina la Emmanuel Mpingwe (32) amefariki dunia baada ya kunywa pombe aina ya gongo kupita kiasi bila ya kula chakula.

Tukio hilo limetokea jana saa tatu usiku Desemba 14 2017 nyumbani kwa James Mwendapole ambaye huwa ni muuza gongo pale kijijini. 

Inasemekana kuwa marehemu alikuwa mlevi wa kupindukia na siku ya Jumatano Desemba 13, 2017 mchana kutwa alishinda akinywa pombe hiyo hadi alipoenda nyumbani kwake kulala na alipoamka asubuhi alirudi tena kuendelea na unywaji wa pombe hiyo pasipo kula chochote. 

Ilipofika muda wa saa 11 jioni, marehemu akiwa amelewa zaidi aliishiwa nguvu na kuzidiwa hivyo watu waliokuwa karibu nae walijaribu kumpa huduma ya kwanza ambayo haikusaidia chochote na hatimaye akafariki dunia.

Aidha, baada ya kufariki dunia, mtuhumiwa Bw. James Mwendapole aliyemuuzia marehemu pombe hiyo kwa siri alitoroka pamoja na mke wake kusikojulikana na kuacha mwili wa marehemu wenyewe.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani humo George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi akiwataka kuungana na jeshi la polisi katika kupambana na biashara haramu ya pombe aina ya gongo pamoja na madawa ya kulevya, kwa kutoa taarifa mapema za watu wote wanaojihusisha kwa siri kwenye biashara hiyo. 

Pombe aina ya gongo ni kinywaji hatari sana kwa afya ya mwanadamu na kina uwezo mkubwa sana wa kudhoofisha afya ya mtumiaji na hata kukatisha maisha

REGIUS NJORA-MASENGWA BLOG

Post a Comment

0 Comments