MWENGE WAIBUA MZOZO BUNGENI
Serikali imesema haina mpango wowote wa kusitisha mbio za mwenge wa uhuru na kwamba dhana ya kutekeleza kitendo hicho kitaendelezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine huku ikiahidi kuwa zoezi hilo litasisitizwa bila kuchoka.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama wakati akijibu swali la Mbunge wa Konde, ndugu Khatib Said Haji aliyekuwa akitaka kujua faida za kuwasha na kuzungushwa kwa mwenge nchi nzima na kama hakuna kwa nini zoezi hilo lisifutwe.
Waziri Mhagama ameendelea kufafanua kwamba Mwenge umesaidia sana katika kukuza ari za maendeleo katika nchi ikiwa ni pamoja na uwekwaji wa mawe ya msingi katika miradi inayoandaliwa na wananchi huku ukiendelea kuhamasisha uzalendo pamoja na umoja ikiwa ni ishara ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere.
"Mtanzania yoyote anayemuenzi baba wa Taifa hili halafu akaukataa Mwenge wa uhuru itabidi tumshangae kwa sababu yeye ndiye muasisi na aliuwasha akiwa ana nia umulike wanyang'anyi, wezi lakini pia uangaze maendeleo, kudumisha amani na mshikamano. Mwenge wa uhuru ni tunu kubwa katika uhuru wa nchi yetu hivyo ni wajibu wa kila mtanzania kuuheshimu mwenge" Mhagama alisisitiza.
Pamoja na hayo Waziri Mhagama amefafanua na kuweka wazi pamoja na dosari ndogo ndogo zinazojitokeza wakati wa ukimbizwaji wa mwenge hazitakuwa chanzo cha kusitisha zoezi hilo bali zitatafutiwa ufumbuzi.
"Dosari ndogo ndogo zinazojitokeza tutazitafutia ufumbuzi lakini siyo kusitisha zoezi la kukimbiza mwenge. Mwenge huu wa uhuru utadumu na utakuwa kama chachu ya maendeleao nchini" aliongeza Mh. Mhagama.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi