SIMBA SC YAPIGWA 2-1 NA KAGERA
SIMBA SC wameshindwa kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuchapwa mabao 2-1 na wenyeji Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba jioni ya jana.
Ushindi huo unaifanya Simba SC ibaki na pointi zake 55 baada ya kucheza mechi 25 na kuwaacha, mabingwa watetezi Yanga SC wakiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi moja zaidi na Kagera Sugar inaendelea kukaa nafasi ya tatu kwa pointi zake za mechi 25.
Katika mchezo huo uliochezeshwa Jimmy Fanuel, aliyesaidiwa na Joseph Masija wa Mwanza na
Geoffrey Msakila wa Geita,hadi mapumziko Kagera Sugar walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Mbaraka Yussuf Abeid dakika ya 27 kwa shuti kali la umbali wa mita 22 baada ya pasi ya mchezaji mwenzake wa zamani wan Simba B, Edward Christopher.
Simba wakaamua kufunguka baada ya bao hilo na kuanza kupeleka mashambulizi ya moja kwa moja langoni mwa Kagera Sugar.
Na Laudit Mavugo, Said Ndemla na Abdi Banda wote wakapoteza nafasi nzuri za kufunga wakiwa wamebaki na kipa Juma Kaseja.
Nafasi ambayo wataijutia zaidi Simba SC ni ya beki Banda dakika ya 43 ambaye alifanikiwa kuipata pasi nzuri ya beki wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na kuwatoka mabeki wawili wa Kagera Sugar, lakini shuti lake dhaifu likadakwa na Kaseja aliyekuwa hatua mbili tu kutoka kwake.
Kipindi cha pili, kila timu ilifanikiwa kupata bao moja, Kagera Sugar wakianza kupitia kwa Edward Christopher aliyemalizia pasi ya Sulemani Mangoma dakika ya 47 kabla ya Muzamil Yassin kuifungia Simba bao la kufutia machozi dakika ya 67 akimalizia pasi ya Mghana, James Kotei.
Baada ya hapo, timu hizo zikaanza kushambuliana kwa zamu na sifa zimuendee kipa mzoefu, Juma Kaseja aliyeokoa michomo kadhaa ya hatari ya Simba.
Kikosi cha Kagera Sugar kilikuwa; Juma Kaseja, Godfrey Taita, Mwaita Gereza, Juma Shemvuni, Mohamed Fakhi, George Kavila, Suleiman Mangoma, Ame Ally ‘Zungu’/Ally Ramadhani, Edward Christopher/Themi Felix, Mbaraka Yusuph na Japhet Makalai/Anthony Matogolo.
Simba leo kipo hivi; Simba SC; Daniel Agyei, Muzamil Yassin, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla/Juma Luizio, Laudit Mavuo, Ibrahim Hajib/Mohammed Ibrahim na James Kotei.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi