Timu ya kudhibiti madawa ya kulevya na mihadarati katika wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, imefanikiwa kulibaini shamba la mahindi lenye ukubwa wa zaidi ya ekari tano, likiwa limechanganywa na zao haramu la bangi lililostawi mno, kwenye msitu wa Lusanzi katika kijiji cha Mawenzusi wilayani humo na kisha kuivuna bangi hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Bw Halfani Haule, akiongelea kuhusu operesheni hiyo iliyowahusisha askari wa majeshi ya polisi, magereza, zimamoto na uhamiaji pamoja na maafisa wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa ya TAKUKURU, amesema imefanikiwa kutokana na ushirikiano mkubwa uliotolewa na jamii kwa kutoa taarifa, ambapo wamefanikiwa kumkamata mtu mmoja anayesadikiwa kulimiliki shamba hilo January Lusambo, na kutoa wito kuendelezwa kwa ushirikiano huo ambao unahitajika mno kufanikisha mapambano hayo.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa kijiji cha Mawenzusi, licha ya kukana kutolijua shamba hilo mapema kwa vile lipo katikati ya msitu huo wa Lusanzi, lakini wameahidi kushirikiana na vyombo vya sheria katika kuwafichua waovu wote wanaojihusisha na kilimo hicho, huku mtuhumiwa wa shamba hilo akikana kata kata kuhusika na shamba.
