Mwanamke huyo, Cleva Mlawizi (33) alifariki Machi 15 usiku na baadaye mwili wake kupelekwa kijijini hapo kwa ajili ya mazishi kwa madai kuwa maelezo ya kifo chake yanatatanisha.
Tukio hilo limetokea wilayani Mbozi, Songwe, mkoa ambao awali ulikuwa sehemu ya Mbeya ambako kumekuwa na matukio ya ajabu, yakiwemo 11 yaliyoripotiwa na gazeti hili wiki iliyopita.
Matukio yaliyotikisa mkoa huo ni pamoja na kuzuka kwa wachuna ngozi za binadamu, wapiga nondo, mauaji ya watoto chini ya miaka mitano, kuzikwa watu wakiwa hai, kukatwa sehemu za siri, kuungua kwa masoko, kuzika jeneza tupu na bwana harusi kumkimbia bibi harusi.
Mengine ni mwanamke kufukua kaburi la mtoto wake, kituo cha maombezi kuwapora mali waumini, kuwapo kwa madhehebu mengi ya dini na mengine kufanya biashara badala ya kutoa huduma za kiroho.
Msemaji wa familia ya mwanamke huyo, Thobias Mlawizi alisema waliamua kuzuia mazishi hayo ili kujiridhisha na mazingira ya kifo cha ndugu yao na kwa mujibu wa maelezo ya mume wa marehemu, hakuumwa bali alifariki ghafla. Maelezo hayo yanatofautiana na ya daktari aliyechunguza mwili huo ambaye alidai alifariki kutokana na njaa.
“Mume wa marehemu anadai walikula wote chakula usiku huo na tukiangalia mwili wa marehemu unavuja damu na umevimba isivyo kawaida,” alisema Mlawizi.
Alisema baada ya kuwapo taarifa zinazotatanisha kuhusu kifo hicho, waliamua kusafirisha mwili wake hadi kijijini hapo na baada ya kufika na kuuona mwili huo ukiwa umevimba huku ukitoka damu, wanadhani ndugu yao alifariki kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Mathias Nyange alisema wahusika walipofika kituo cha polisi walifanya mawasiliano na wenzao wa Sumbawanga na kuelezwa kwamba iwapo hawakuridhika na uchunguzi wa awali, waupeleke mwili wa marehemu Hospitali ya Rufaa jijini Mbeya ili ufanyiwe uchunguzi mwingine.
