Siku chache baada ya Mfanyabiashara na Diwani wa Mbagala Kuu Yusuf Manji kuachiliwa kwa dhamana kwa tuhuma za kujihusisha na baishara ya dawa za kulevya, amewasilisha maomba Mahakama Kuu ikiiomba iwaagize maafisa wa Uhamiaji wamfikishe mahakamani ili kesi yake inayomkabili iweze kusikilizwa.
Februari 20 mwaka huu Manji alifikishwa katika ofisi za uhamiaji jijini Dar es Salaam na kufanyiwa mahojiano akituhumiwa kuingia nchini kinyume na sheria.
Kuanzia wakati huo, amekuwa chini ya ulinzi wa polisi katika hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam ambapo anapatiwa matibabu.
Maombi hayo yaliyowasilishwa na mwanasheria wa Yusuf Manji yanalengo la kuwataka Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Ofisa wa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam wamfikishe mteja wake mahakamani, kesi isikilizwe ili haki yake iweze kupatikana.
Manji baada ya kuhojiwa katika ofisi za uhamiaji kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume na sheria na hivyo kuwa si raia halali wa Tanzania, alirejeshwa katika Hospitali ya Aga Khan ambapo yupo hadi leo