YANGA YAZIDI KUMPA UMAARUFU KICHUYA
Yanga imeendelea kumpa umaarufu mkubwa kiungo mshambuliaji Shiza Kichuya baada ya kumruhusu kuwatungua mara mbili mfululizo kwenye mechi za ligi kuu Tanzania bara, magoli yote ambayo Kichuya amewafunga Yanga ni ya ajabu na yamekuwa muhimu sana kwenye matokeo ya Simba.
Kichuya alipiga pasi ya mwisho (assist) iliyomkuta Laudit Mavugo kwenye nafasi na kupasia nyavu kwa kichwa. Goli hilo lilizaliwa baada ya wachezaji wa Simba kugongeana pasi kuanzia kwa Ndemla ambaye alipiga pasi kwa Kichuya, kichya akamuwekea Mzamiru kisha Kichuya akaiomba tena akapewa na Mzamiru ambapo alipiga krosi ya juu ikamkuta Mavugo kwenye nafasi na kuruka juu akimzidi beki wa Yanga Vicent Andrew ‘Dante’ na kuzamisha mpira kambani.
Goli hilo likawapa Simba morali wakajipanga kwa ajili ya kupata bao jingine na wakafanikiwa kufunga goli la pili na la ushindi kwao.
Kichuya alifunga goli la ushindi kwenye mchezo wa jana likiwa ni goli lake la pili mfululizo kwa Yanga tangu ajiunge Simba akitokea Mtibwa Sugar. Kichuya alifunga goli hilo upande uleule alikofunga goli lake kwenye raundi ya kwanza (upande wa Kaskazini Mashariki). Kichuya alifunga goli hilo baada ya kupokea pasi kutoka kwa nahodha Jonas Mkude kisha akasogeza mara mbili na kuuzungusha (ndizi) mpira akiwa nje ya eneo la penati box na mpira ukazama nyavuni ukimwacha Dida akiruka bila mafanikio.
Mchezaji huyo mzaliwa wa Morogoro, mechi ya raundi ya kwanza alimfunga Barthez kwa kona iliyozama moja kwa moja wavuni na kuisawazishia Simba iliyokuwa nyuma kwa goli 1-0 wakati huo wakiwa pungufu baada ya Jonas Mkude kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya.
Goli hilo ni kama limemrudisha Kichuya ambaye alikuwa hajafunga kwa muda mrefu na mechi kadhaa amekuwa akianzia benchi. Kichuya anafikisha magoli 10 kwenye orodha ya wafungaji wa ligi kuu Tanzania bara goli moja nyuma ya Msuva anayeongoza akiwa na magoli 11 hadi sasa.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi