WAFANYAKAZI WA YUSUPH MANJI WAFIKISHWA MAHAKAMANI
Raia 14 wa India ambao wanafanya kazi Quality Group iliyo chini ya Yusuf Manji leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu likiwemo la kufanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.
Hati ya mashtaka, iliyosomwa na mwendesha Mashtaka, wa uhamiaji Method Kagoma imewataja washtakiwa hao kuwa ni Rojat Surkar, Jagadish Mamidu, Niladri Maiti, Sivarar Raja Sekaran, Mohammed Taher Shaikh, Bijenda Kumar, Prasoon Kumar Mallik na Nipun Dinbandhu Bhatt.
Wengine ni Pintu Kumar, Anuj Agurwa, Varun Boloor, Arun Kumar Kateel, Avinash Chandratiwari na Vikram Sankhala.
Akisoma hati ya mashtaka, Kagoma amedai kuwa, Februari 13, mwaka huu, huko katika ofisi ya Quality Group Ltd iliyopo katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikutwa wakiwa na viza zilozoghushiwa za kufanyia kazi.
Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa siku na mahali hapo washtakiwa hao wakiwa raia wa India walikutwa wakiishi nchini Tanzania bila ya kuwa na kibali.
Kagoma aliongeza kuwa, Februari 13 mwaka huu, katika jengo la Quality Group washtakiwa hao wakiwa raia wa India walikutwa wakijihusisha na kufanya kazi katika kampuni hiyo kama washauri bila ya kuwa na kibali cha kufanya kazi nchini.
Hata hivyo, washtakiwa hao ambao wanatetewa na mawakili watatu, Alex Mgongolwa na Hudson Ndusyepo wamekanusha kujihusisha na tuhuma hizo na wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Mahakama iliwaamuru washtakiwa hao kuweka dhamana ya milioni tano kila mmoja na kuleta mdhamini mmoja kila mtu atakayeweka kiasi hicho cha fedha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 7, mwaka huu.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi