NDUGU WABADILISHIWA MAITI HOSPITALI KATAVI



VURUMAI kubwa na taharuki imetokea jana katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi baada ya ndugu wa marehemu Mathias Madega, kukabidhiwa maiti ambayo siyo ya ndugu yao.

Hali hiyo ilitokana na watumishi wa afya kuuchukua mwili wa ndugu yao huyo na kuwakabidhi watumishi wa Manispaa na kwenda kuuzika kwa madai kuwa haukuwa na ndugu.

Tukio hilo lililovutia hisia za watu wengi wa mji wa Mpanda, lilitokea saa 8:00 mchana baada ya ndugu wa Madega kufika katika chumba cha kuhifadhi maiti kwa lengo la kuuchukua mwili wa mpendwa wao kwa ajili ya maziko kulingana na taratibu za familia yao.

Baada ya wafiwa wakiongozwa na baba mdogo wa marehemu, George Madega, kufika katika hoaspitali hiyo, walimkuta muuguzi ambaye waliongozana naye mpaka chumba cha kuhifadhi maiti kisha akawaonyesha maiti moja iliyokuwamo akidai kuwa ni ya ndugu yao hivyo wachukue kwa maziko.

Maiti waliyoifuata, ilikuwa imehifadhiwa kwa siku mbili, lakini maiti waliyoonyeshwa, ilikuwa imeharibika vibaya na kutoa harufu kali ikiashiria ni ya siku nyingi.

Majokofu ya chumba cha hifadhi ya maiti katika hospitali hiyo yameharibika.

Hata hivyo, baada ya kuifanyia ukaguzi maiti ile, walibaini kuwa si ya ndugu yao, kitendo kilichowakasirisha na kumujia juu muuguzi ambaye baada ya kuwaonyesha mwili huo, alirudi nje kukwepa harufu.

Muuguzi huyo aliwaeleza wafiwa hao kuwa watumishi wa Manispaa, walikwenda hospitali hapo na kuuchukua mwili wakidhani ni wa yule asiye na ndugu na kwenda kuuzika.

Kwa msingi huo, wafiwa hao walibaini kuwa maiti iliyokwenda kuzikwa na watumishi wa Manispaa, ndiyo ya ndugu yao.

Ndipo walipoanza kufuata taratibu za kisheria na kisha mahakama ikatoa kibali kwenda kufukua kaburi na kukuta aliyezikwa ni ndugu yao.

Wafiwa hao waliuchukua mwili huo na kwenda kuuzika kwa taratibu za familia yao.

Mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali hiyo, George Nsalamba, alisema siku ya tukio hakuwapo.

Nsalamba alisema kosa hilo la kuchanganya maiti lilifanywa na aliowaachia funguo za chumba cha hifadhi ya maiti akimtaja muuguzi aliyekwenda kusimamia utoaji wa maiti ya kwanza ambayo ilizikwa na Manispaa.

Aidha, mazishi ya Madega yamepangwa kufanyika leo katika makaburi ya Misunkumilo Manispaa ya Mpanda.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa baada ya mahakama kutoa kibali cha kufukua kaburi, ndugu wa marehemu walikubali kuwa ni mwili wa ndugu yao.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.