HIVI HAPA VITUKO VILIVYOTAWALA KWENYE MECHI YA SIMBA NA YANGA
Miaka yote, mechi ya Simba na Yanga hutawaliwa na matukio mengi, kebehi, majivuno na mambo mengine achilia mbali matokeo baada ya mechi lakini pia vituko vya wachezaji huwa havikosekani.
Katika mchezo wa jana kabla ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, wacheza wa Yanga waliingia kwa mkwara uwanjani na kuondoka kimya kimya huku kibao kikigeukia kwa wale wa Simba.
Yanga iliwasili uwanjani saa 8:50 kwa mbwembwe ikiongozwa na king'ora cha polisi na basi la wachezaji lilitanguliwa na magari mengine manne.
Msafara huo ulisimamisha kwa muda shughuli zilizokuwa zikiendelea nje ya uwanja huku moja ya magari manne ya maji ya kuwasha yaliyokuwa uwanjani hapo likilifuatilia basi la wachezaji wakati msafara unaingia hadi wachezaji walipoingia vyumbani.
king'ora cha Simba baada ya mechi
Simba iliyowasili uwanjani saa 8:21 ilikuja kimya kimya bila king'ora, lakini baada ya ushindi timu yao ilitoka uwanjani na king'ora huku mashabiki wakilisukuma basi la wachezaji.
Msafara huo ulizunguka kwa dakika kadhaa katika maeneo ya Uwanja wa Taifa kupitia Chuo Kikuu cha Ualimu, Duce na kisha kurejea tena uwanjani huku mashabiki wakiendelea kulisukuma hadi unapoishia Uwanja wa Uhuru na kuliacha basi hilo ambalo lilipitia Barabara ya Kilwa.
Milango ya kuingilia yabadilika
Katika mechi ya juzi, wachezaji wa pande zote mbili walibadili njia za kuingilia vyumbani.
Simba ndiyo walikuwa wa kwanza baada ya kutumia mlango mdogo wa kuingilia uwanjani uliopo upande wa kushoto.
Wakati timu inaingia, baadhi ya viongozi wa Simba akiwamo rais, Evance Aveva walikuwa katika mlango mkuu wa vioo wa kuingia uwanjani wakiwatazama kwa mbali na kisha na wao kuingia kwa mlango tofauti na kuwafuata wachezaji vyumbani.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi