DC AAGIZA 'TIGER' NA WENZAKE WAKAMATWE
WAKAZI wa Kata ya Kinondoni katika Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam wamelalamikia kuwepo kwa wahalifu wanaokaba na kuwanyang’anya watu mali wakiongozwa na mtu anayeitwa Rama maarufu kwa jina la Tiger.
Mbali na Tiger, wahalifu wengine waliotajwa kusumbua wananchi hao ni Ali maarufu kama Kijiwe na Chamsela ambao wamekuwa wakifanya uhalifu hadi nyakati za mchana na polisi wamekuwa wakiwakamata na kuwaachia.
Malalamiko hayo yalitolewa na wananchi hao katika mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi uliofanyika Mtaa wa Ufipa, Kata ya Kinondoni wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.
Baada ya kupokea malalamiko hayo, mkuu wa wilaya ameagiza Polisi wilayani humo kuhakikisha wanawakamata wahalifu wote na kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria.
“Huyu Tiger ni nani katika wilaya yangu hadi awakamate na kuwanyanyasa wananchi, sasa naagiza huyo mtu akamatwe na wahalifu wengine wote wakamatwe, Kamanda fuatilia haya malalamiko,” ameagiza Hapi.
Hapi pia amemuagiza Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Gerald Ngiichi kufuatilia malalamiko ya wananchi hao waliodai kuwa wapo baadhi ya watu wanakamatwa bila makosa, huku akiwataka wananchi hao kutotetea wahalifu hata kama ni watoto wao.
“Hakuna Kinondoni ya wazawa wala wakuja, ukikaa hata kama ni kibarazani unavuta bangi au unakula mirungi wewe ni mhalifu, kamateni hawa walioko kwenye hivi vijiwe wanaojiita wazawa,” amesema.
Awali, wananchi hao walilalamika kuwa baadhi ya polisi wamekuwa wakishindwa kuwa waadilifu kwani wamekuwa wakiwakamata wahalifu na kuwaachia baada ya kupewa rushwa.
Akijibu malalamiko hayo, Kamanda Ngiichi alisema watafuatilia malalamiko hayo na kuchukua hatua huku akiwataka wananchi wa maeneo hayo kufichua uhalifu kwani wapo baadhi yao wamekuwa wakiwatetea watoto wao wanaojihusisha na uhalifu.
“Tatizo sio kukamata, tatizo ni ushahidi tunawakamata hawa wahalifu na tunawapeleka mahakamani lakini watu wanapoitwa kutoa ushahidi hawaji mahakamani, sasa hili ni tatizo na ndio unakuta wanaachiwa,” amesema Kamanda Ngiichi.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka polisi kuhakikisha wanafanya operesheni za mara kwa mara ili kumaliza tatizo la uhalifu katika wilaya hiyo
Chanzo Habari Leo
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi