ASKOFU MOKIWA AFUNGUA KESI
ALIYEKUWA Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa, amefungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akiiomba itengue uamuzi wa kuvuliwa uaskofu na kumtangaza kuwa askofu.
Dk. Mokiwa kwa kupitia kampuni ya uwakili ya M. B Kabunga and Co. Advocates, Mathew Kabunga, alifungua kesi hiyo namba 20 ya mwaka huu, dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya na bodi ya wadhamini ya kanisa hilo, akipinga kuvuliwa uaskofu.
Shauri hilo lililoko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, limepangwa kutajwa mahakamani hapo Februari 28, mwaka huu, hata hivyo mawakili wa kanisa hilo, Gabriel Masingwa na Emmanuel Nkoma, jana walitinga mahakamani hapo.
Mawakili hao walifika mbele ya Hakimu Simba, wakidai kwamba walipewa maelezo ya kutakiwa kufika mahakamani hapo, ambapo Hakimu Simba alisema katika kumbukumbu za kesi shauri hilo limepangwa Februari 28, mwaka huu.
Mawakili hao walieleza kuwa walipatiwa barua kutoka na wakili wa Dk. Mokiwa, M. B Kabunga, hata hivyo upande wa mlalamikaji hawakuwepo mahakamani hapo licha ya kuwapatia walalamikaji barua ikionesha kwamba kuna jitihada za kumaliza mgogoro huo katika nyumba ya maaskofu.
“Hapa mahakamani kuna hati ya madai na hati ya kujibu madai na kesi ilishapangwa kuja Februari 28, mwaka huu, hivyo kwa leo siwatambui na siwezi kuingiza chochote katika kumbukumbu za mahakama,” alisema Hakimu Simba.
Kwa mujibu wa barua hiyo kutoka kwa wakili wa Dk. Mokiwa, anaomba tarehe ya kutajwa kwa shauri hilo, irudishwe nyuma kwa kuwa kuna juhudi za kutatua mgogoro katika nyumba ya maaskofu.
Barua hiyo, inaeleza kutokana na hilo, wakili huyo ameelekezwa na mteja wake kuondoa shauri hilo mahakamani kwa kuwa utaratibu wa kumaliza mgogoro huo haiwezi kufanyika isipokuwa kuondoa kesi.
Dk. Mokiwa baada ya kufungua kesi hiyo, mawakili wa kanisa hilo, waliamua kuwasilisha mahakamani hapo majibu yao, wakiiomba kuitupilia mbali kesi hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kuisikiliza.
Kwa kupitia hati yake ya maadai, Dk. Mokiwa anadai kwamba waumini takriban 28 wa kanisa hilo, waliandika barua ikiwa na mashitaka 10 dhidi yake, lakini barua hiyo haikuwasilishwa kwake na kwake ilionesha kuna nakala.
Anadai kwamba Desemba 20, mwaka jana, mlalamikiwa wa kwanza (Dk. Chimeledya) alimuandikia barua kumtaka kustaafu mwenyewe katika nafasi yake bila ya kueleza sababu na kumpa nafasi ya kuweza kujibu tuhuma.
Kwa kupitia hati yake ya madai, Dk. Mokiwa anadai kwamba tuhuma hizo hazina vielelezo vyovyote vya kuthibitisha tuhuma hizo, bali ni mambo ya kupika kumualibia askofu huyo. Kutokana na hayo, anaiomba mahakama kuamuru Dk. Mokiwa ni askofu halali, kumlipa gharama za kesi na kutoa amri nyingine inazoona zinafaa.
Katika hati yao ya majibu, walalamikiwa hao wanadai hati ya madai haipo sahihi mahakamani hapo, kwa kuwa haina uwezo wa kuingilia masuala ya kiimani kwani yanapaswa kusikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi kwenye vyombo vya kidini.
Aidha, wanadai kitendo cha Dk. Mokiwa kufungua kesi hiyo mahakamani ni kwenda kinyume na Katiba ya Kanisa la Anglikana ya mwaka 1970 ambayo ilifanyiwa marekebisho Oktoba, 2014. Januari 7, mwaka huu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk. Chimeledya alimvua uaskofu mkuu Dk. Mokiwa kutokana na mashitaka 10 aliyofunguliwa na walei 32 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa.
Uamuzi wa kumvua uaskofu ulichukuliwa baada ya Dk. Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauriwa na nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini Licha ya uamuzi wa kumvua uaskofu, Dk. Chimeledya pia aliagiza waraka unaoagiza askofu huyo kuondolewa madarakani, usambazwe kwenye makanisa yote yaliyoko chini ya dayosisi ya Dar es Salaam na usomwe jana kwenye ibada mbele ya waumini.
Hata hivyo, Dk. Mokiwa aliugomea uamuzi huo kwa maelezo kuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Saalam ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na sio askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania.
Dk. Mokiwa alikuwa akituhumiwa kuzuia dayosisi ya Dar es Salaam kupeleka michango pasipo maelekezo ya sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, kuhamasisha dayosisi kujitoa katika udhamini wa kanisa Anglikana Tanzania (KAT) kwa lengo la kuifarakanisha dayosisi na jimbo kinyume na katiba ya dayosisi.
Mashitaka mengine ni kufuja mali za kanisa na kuingia mikataba kiholela yenye viashiria vya rushwa katika eneo la kanisa la mtoni Buza na miradi mingine, kushindwa kutatua migogoro inayohusu uwekezaji na maadili baina ya dayosisi na mitaa ya Magomeni ambao kuna mgogoro na Benki ya DCB, kanisa la Kurasini na mengine.
Askofu huyo pia anadaiwa kushindwa kutatua migogoro baina ya mapadiri na waumini na kutunza mali za kanisa katika mtaa wa Watakatifu wote Temeke na kutelekeza nyumba ya askofu iliyopo Oysterbay ambako imegeuzwa kuwa yadi ya kuuza magari.
Pia alilalamikiwa kushitakiwa mahakamani na Marehemu Christopher Mtikila na watu wengine watatu kwa kosa la kuwatishia silaha ya moto na kuwapapasa maungoni mwao bila ridhaa yao kinyume na maadili ya kikanisa.
Askofu Mokiwa pia analalamikiwa kuanzisha taasisi ya MEA Foundation iliyomwezesha kupokea fedha nyingi za wafadhili kwa ajili ya maendeleo ya dayosisi, lakini fedha zimefujwa na hesabu za chombo hazikuwahi kukaguliwa.
Tuhuma zingine ni kurejea kwa mchakato wa mapitio ya katiba mpya na kuvuruga mchakato wa awali wa maandalizi ya katiba mpya ya dayosisi kwa kutumia fedha za dayosisi na kutekelezwa askofu msaidizi dayososi ya Katanga Kalemi Maamuzi ya nyumba ya maaskofu Kwa mujibu wa waraka huo ambao unafafanua hatua zilizopitiwa hadi kuchukua hatua ya kumvua uaskofu, unaeleza kuwa halmashauri ya kanisa la Anglikana Tanzania ilibaini kuwa askofu Mokiwa alivunja sheria za nchi na hivyo kuhatarisha kanisa kupoteza mali zake au kushitakiwa mahakamani kwa kuruhusu mabadiliko ya matumzi ya ardhi katika shamba la kanisa la Mtoni Buza eneo la kanisa la St Mariam Kurasini.
Chombo hicho pia kilisema Dk Mokiwa alikiuka na kuvunja sheria ya miunganiko ya udhamini ya katiba ya kanisa Anglikana Tanzania na katiba ya Dayosisi ya Dar es Salaam kwa kutia saini na kuruhusu padri John Mhina ambaye sio mdhamni kutia saini mikataba mikubwa ya uwekezaji katika maeneo ya kanisa anglikana bila kuweka muhuri wala kushirikisha wadhamini.
Halmshauri pia ilibaini askofu Mokiwa ameshindwa kutimiza wajibu wake wa uaskofu wake kwa kutelekeza mali za kanisa na kuziacha ziharibike ikiwemo nyumba ya askofu iliyoko Oystebay, Nyumba ya kanisa ya Silver Oak na shamba la Buza.
Alikutwa na hatia ya kutumia vibaya madaraka yake kwa kushindwa kusimamia mikaaba ya uwekezaji katika shamba la kanisa la mtoni Buza, Magomeni na Kurasini. Pia alikutwa na hatia ya kutumia vibaya vyombo vya mamuzi vya dayosisi ili kuhalalisha na kupitisha maamuzia mbayo yalilenga kulidhoofisha kanisa Angalikana Tanzania kwa maslahi binafsi.
Nyumba ya maaskofu pia ilimkuta na hatia ya ufisadi kwa kuruhusu kufunguliwa akaunti yenye jina la Diocese of Dar es Salaam Evangelism katika benki ya ACB ambayo iliingia fedha nyingi na fedha hizo zimetumika zote katika muda mfupi na haijulikani matumizi yake. Yeye alikuwa mtia saini wa akaunti hiyo na baadhi ya wasaidizi wake.
“Nyumba ya maaskofu iliona kuwa lipo kosa kubwa lililofanywa na baba askofu Mokiwa ya kuvunja sheria za nchi na yeye mwenyewe alikiri shitaka linalohusu mikataba mibovu na matumiz mabyaa ya fedha za kanisa,” inasema barua hiyo
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi