Waziri Muhongo asitisha bei mpya ya umeme
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kusitisha bei mpya ya umeme iliyotangazwa juzi na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Felix Ngamlamgosi.
Taarifa ya kusitisha kwa bei hiyo ilitolewa jana na Profesa Muhongo kupitia barua yake kwa Ewura.
Muhongo amesema kuwa amesitisha bei hiyo mpya kwa sababu nne, ikiwamo kutoshirikishwa katika mchakato huo akiwa ni waziri mwenye dhamana.
“Ewura walipokwenda mikoani Watanzania wote walipinga bei kupanda, wao wametumia kigezo kipi cha kupandisha? Pili taratibu zilizopo ni kwamba Tanesco wanapeleka maombi Ewura, kisha Ewura wanafanya zoezi hilo la kuuliza wahusika watumiaji wa umeme, baada ya hapo wanatengeneza ripoti wanaileta wizarani, na ningaliipata hiyo ripoti.
“Hivi tunavyoongea sijaipata mkononi, nikiipata nitaiita Ewura na Tanesco tunajadili na baada ya hapo ndipo wanaenda kutangaza. Wao wametangaza hata mimi taarifa nazipata kama wewe,” alisema Profesa Muhongo.
Katika sababu ya tatu ya kusitisha bei hiyo, Profesa Muhongo alisema hakuna ukweli kuwa kupandisha bei ya umeme kutasababisha Tanesco imalize matatizo yake kifedha.
“Tanesco kila mwaka inapandisha bei, mbona hawajajikwamua? Mbona madeni yanazidi kuongezeka? Nyingine ni kwamba tunakopa fedha kutoka nje ya nchi na watakaolipa hilo deni ni Watanzania wote, sasa hatuwezi kukopa kulipa madeni ya Tanesco halafu shukrani tutakayoipata ni kupandishiwa bei ya umeme tena.
“Nyingine nenda ufuatilie Tanesco wana matumizi mabaya ya fedha, nimesitisha zoezi lao, sijui kama hizo fedha wamerudisha, unajua wanapeana wale walioko juu bonasi kati ya Sh milioni 40 na milioni 60 kwa mwaka,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema Ewura wanapaswa kupeleka ripoti ijadiliwe, kwani haiwezi kuwa Serikali ndani ya Serikali na haiwezi kupandisha bei bila waziri mwenye dhamana kujua kwa kuwa inapata bajeti kutoka bungeni.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi