Maalim Seif na Lowasa kuunguruma Zanzibar Jumapili hii
Wanasiasa wakongwe nchini, Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika, kesho wanatarajia kuungana kwa mara ya kwanza jukwaani tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Vigogo hao wa vyama vya CUF (Maalim Seif) na Chadema (Lowassa) wataunguruma katika viwanja vya Skuli ya Fuoni visiwani Zanzibar kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani, katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januri 22 kuziba nafasi ya aliyekua mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ally Tahir aliyefariki dunia Novemba 11 mwaka jana.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu amesema kuwa chama chake kimemua kuungana na CUF katika uchaguzi huo ili kuhakikisha mshirika wake huyo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) anamshinda mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, Mwalimu aliongeza kuwa baada ya Lowassa kushiriki uzinduzi wa kampeni hizo kesho, viongozi wengine wa Chadema watafuata kwa kufanya mikutano mbalimbali jimboni humo. Alisema kuwa baada ya Lowassa atafuata Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja Tundu Lissu kwa nyakati tofauti, kisha wengine wataendelea hadi mwisho wa kampeni hizo.
Akizungumzia uamuzi huo wa Chadema, Mkurugenzi wa Habari,Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Salim Bimani alieleza kufurahishwa na uamuzi huo wa Chadema na kueleza kuwa hatua ya Lowassa kuhudhuria uzinduzi huo itaongeza hamasa kubwa kwa wapenzi wa chama hicho.
“Umenambia hadi Lowassa atakuwepo? Ni furaha iliyoje, Wanzibari wana shauku kumuona. Siku ya kampeni patakuwa hapatoshi Skuli ya Fuoni, hapa Simba (Maalim Seif) kule Lowassa kipenzi kingine cha Wazanzibar,” Bimani anakaririwa na Mwananchi.
Aliongeza kuwa kama Lowassa atahudhuria mkutano huo atakuwa na mambo mawili makubwa ya kufanya, la kwanza likiwa kuwashukuru Wazanzibar kwa kura walizompa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Na la pili litakuwa kumpigia kampeni mgombea wa CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani.
Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, wataingia katika jimbo hilo ikiwa ni siku chache baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kufanya uzinduzi wa kampeni hizo akiambatana na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho.
Hivyo, kwa muktadha wa kisiasa, vigogo hao wa Ukawa wana kazi ya kusawazisha matuta yaliyowekwa na timu ya chama tawala iliyoongozwa na Kinana.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi