Mwambe amesema kuwa binti huyo mwenye umri wa miaka 14 (jina limehifadhiwa) alifunga ndoa ya kimila na Jeremiah Anthony (20) ambaye ni fundi mwashi nyumbani kwa mama mzazi wa bwana harusi eneo la Mwanzi, mjini Manyoni.
Alisema aliweza kupata taarifa hizo kupitia kwa wenyeviti wa vitongoji vya Samaria na Mwanzi, Mtendaji Kata na Diwani wa Manyoni na kuzifanyia kazi mara moja.
“Binti huyo ana tatizo la kifafa. Wazazi walitumia kigezo cha ugonjwa wake kumkatiza masomo na kumuozesha ili kuondokana na shida,” alisema.
Kufuatia tukio hilo, alisema bwana harusi Jeremiah, mama wa bwana harusi Janeth Makole na kaka wa bwana harusi Alexander Anthony wamefikishwa polisi kwa uchunguzi zaidi wakati wazazi wa mwanafunzi huyo, baba na mama Robert Mlewa wanaendelea kutafutwa.
“Ndoa tayari ilishafungwa kwa wazazi wa bwana harusi huko Mwanzi na sherehe ya harusi hiyo ilikuwa ifanyike mjini hapa Manyoni. Tumewakamata mama mzazi wa Jeremiah, kaka yake na yeye bwana harusi. Nimeagiza afunguliwe shitaka la kubaka,” alisema Mwambe.
Aidha, nimeagiza arudishwe shule akaendelee na masomo, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya wilaya ya Manyoni amlipie gharama za sare na vifaa vya shule na Ofisa elimu na Ofisa Maendeleo ya Jamii wamsimamie na wawe walezi wake kuhakikisha anafika mbali kielimu.
