
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Monduli mkoani
Arusha, Loota Sanare amesema halmashauri ya wilaya hiyo inayoongozwa na
Chadema, inachochea migogoro ya ardhi na chama hakitakaa kimya kwa hilo.
Sanare alisema hayo juzi katika mkutano wa hadhara wa kijiji cha
Lendikinya, uliohudhuriwa na vijana wa jamii ya Kimasai (morani) na
wazee wa mila (Laigwanani) zaidi ya 300, kueleza ardhi ya kijiji hicho
inayotaka kunyang’anywa na halmashauri hiyo.
Alisema vijana wa kimorani, Laigwanani na watu wengine akiwemo yeye
mwenyewe Sanare, wanamiliki ardhi iliyopo katika kijiji hicho kwa
kufuata michakato yote ya kisheria na hatimaye kupata hati ya kumiliki
ardhi.
Alisema amesikitishwa na kauli ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Monduli, Isack Joseph kutangaza baadhi ya watu kuwa wanamiliki ardhi
katika msitu huo kinyume cha sheria.
Alisema CCM haitavumilia uchochezi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa halmashauri kwa maslahi binafsi.
Pia, alisema CCM haitavumilia kuona mwananchi yeyote anaonewa.
Sanare alisema yeye alipata shamba hilo kama mwananchi wa kijiji
hicho na hakuchukua shamba hilo kama kiongozi wa CCM. Alisema kitendo
cha kuingiza chama katika mambo yake binafsi kimemsikitisha, hivyo na
yeye hatavumilia hayo.
Alisema si yeye tu anayemiliki ardhi katika kijiji hicho, kwani hata
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa (Waziri Mkuu mstaafu)
ana ekari za kutosha katika eneo hilo pamoja na diwani wa Monduli Juu na
wengine walioko ndani ya Chadema.
Lakini, alisema hao wote hawakuguswa, kwa sababu ni wana Chadema.
Alidai huo ni ubaguzi na uchochezi na unapaswa kupigwa vita. Mjumbe
wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Monduli, Amani Ole Silanga, aliwataka
wanakijiji kuwa na subira, kwani huo ni upepo mchafu unaovuma kupitia
baadhi ya viongozi wa halmashauri na baraza la madiwani.
Alisisitiza kuwa upepo huo mchafu utapita. Laigwanani, Oleleku Ndeese
aliitaka CCM kusimamia hilo kwani Chadema iko Monduli kutaka kupora
haki za watu na hilo halitavumilika kamwe na ameomba wasaidie damu
isimwagike.
Morani, Songoro Matata alihamasisha wanakijiji walioko kwenye vyama
vya siasa kupima na kuona ni chama gani kipo kutetea maslahi ya wananchi
na kukifuata chama hicho.
Hivi karibuni Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Monduli,
lilipitisha azimio la kuchukua ardhi ya kijiji hicho kwa madai kuwa
waliochukua ardhi hiyo hawakufuata sheria, akiwemo mwenyekiti wa CCM wa
wilaya hiyo
CHANZO - HABARI LEO