Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Dr. Emmanuel Joseph Makala, ametoa wito kwa wakristo na watanzania wote kwa ujumla kupanda mazao yanayostahimili ukame hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na uhaba mkubwa wa mvua uliosababisha mazao mengi yaliyopandwa kukauka.
Akizungumza na wakristo katika ibada iliyofanyika jana katika kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Ebeneezer Kanisa Kuu Shinyanga, askofu huyo amewasihi kuzitumia mvua zinazoendelea kunyesha sasa kwa kupanda mazao yanayostahimili ukame kama mtama ili kuweza kukabiliana na hali ya upungufu wa chakula nchini.
Pia kutokana na uoto wa asili kuzidi kupotea kila kukicha, askofu amewasihi wakristo kupanda mti angalau mmoja kwa kila kaya ili kujaribu kurudishia uoto huo kwani miti ni chanzo kikubwa cha kuleta mvua.
Katika ibada hiyo, wakristo wa dhehebu hilo walifanya maombi ya kuombea mvua wakitekeleza agizo lililotolewa na mkuu wa kanisa la KKKT Askofu Dr. Fredrick Shoo.