Ajinyonga baada ya mama kumzuia asimrithi shemejiye


Rorya. Mkazi wa Kijiji cha Muharango, Kata ya Nyamagaro wilayani hapa, Lukas Jenge (24)  amefariki dunia kwa kujinyonga na kamba ya katani baada ya mama yake kumzuia asimrithi shemeji yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Andrew Satta alisema tukio hilo lilitokea Januari 21 majira ya saa tano usiku.

Satta alisema kijana huyo aliamua kujiua baada ya mama yake kumtaka aachane na shemeji yake aliyekuwa amemrithi kutokana na kifo cha kaka yake kilichotokea mwaka jana.

“Haya ni mambo ya kijamii wazazi wanaweza kuwa chanzo, mila na desturi zinaweza kuwa chanzo cha matatizo haya, lakini pia jamii tushiriki kuiasa,” alisema.

Kamanda huyo aliwataka  wazazi kusimamia mambo ya msingi katika jamii.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jumanne Mkirya alisema kitendo cha mama kumweleza mara kwa mara mwanaye aachane na shemeji yake kilimfanya achukue uamuzi huo mgumu kama kumkomoa mzazi wake.

Mkirya alisema kabla ya kijana huyo kuanza kuishi na shemeji yake kama mkewe, pia alikuwa na mke mwingi aliyemuoa siku nyingi zilizopita. “Nilipigiwa simu usiku kuwa kuna mtu amefariki kwa kujinyonga na nilipofika nilimkuta amekwishakufa ikabidi tukate kamba na kutoa taarifa polisi ambao walifika na kumchukua kwa uchunguzi zaidi,” alisema.

Alisema kuwa kijiji hicho kimekuwa na matukio mengi ya wananchi kujinyonga na kwamba, inahitajika elimu  ili kuondoa dhana ya kujimaliza. “Watu wamejijengea ya kuwa njia ya kutatua matatizo yao ni kujinyonga au kunywa sumu. Matukio ni mengi. Wapo wengine wanapona na kuendelea kuishi, lakini tunaomba wanaponusurika wachukuliwe hatua kwa kitendo kile,” alisema Mkirya.

Pia, mwenyekiti huyo aliwataka wazazi kutoingilia uamuzi wa watoto kwani tayari wanakuwa wameamua juu ya maisha yao.

Wakati huohuo, katika Kitongoji cha Nyangabo, Kijiji cha Nyang’ombe, Babu Greeni (24) amefariki dunia kwa kunywa sumu.

Mjomba na marehemu, Mourice Kayaka alidai kuwa baada ya kufariki dunia kwa mama wa kijana huyo, Greeni aliondoka kwenda kumtafuta baba yake mzazi hadi mauti yalipomkuta. “Nilishamsahau maana aliondoka tangu akiwa mdogo hata sijui kama amefariki wala kama amezikwa,” alisema na kuongeza kuwa:

“Dada yangu baada ya kuolewa na mume mwingine, kijana huyo aliondoka nyumbani kwenda kumtafuta baba yake tangu hapo hatukuwahi kumwona.”