Kigogo mamlaka ya Elimu atumbuliwa kimya kimya
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata jana kutoka chanzo cha kuaminika zinasema kwamba, Laurent amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa Sh bilioni 36 za mamlaka hiyo.
“Ni kweli amesimamishwa ili kupisha uchunguzi ambao tunaamini unahusiana na kauli ya Rais Dk. John Magufuli kuwa kuna Sh bilioni 36 zimewekwa katika akaunti maalumu (Fixed Deposit Account) benki za biashara,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo chanzo hicho kilisema kuwa, hadi Novemba 24 mwaka huu mamlaka hiyo ilikuwa na Sh bilioni 2.3 tu katika Benki ya ACB.
“Zilikuwa zikikatwa asimilia 14 ya riba na Sh bilioni 29 tayari zimehamishiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambako kuna akaunti ya mamlaka kwa ajili ya kununua hati fungani,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kilisema fedha hizo zilikuwa zimenunua hati fungani kwa asilimia 14. “Aprili mwaka huu ofisi ya TEA ilimwandikia barua Msajili wa Hazina kutaka kupewa maelekezo ya kufungua akaunti pale BoT, tunashukuru mambo yalikwenda vizuri,” kilisema chanzo hicho.
Laurent aliteuliwa Oktoba, 2015 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo, baada ya kukaimu kwa muda mrefu.
Akiwa katika maafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Rais Magufuli alisema TEA ilianzishwa kwa sababu maalumu na imekuwa ikichangiwa fedha wakati kuna fedha zao wameziweka kwenye akaunti maalumu na kumtaka Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolijia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuchukua hatua.
“Hata kwa sasa waziri uko hapa, Mamlaka ya Elimu Tanzania ilianzishwa kwa sababu maalumu inachangiwa fedha wakati zao wameweka kwenye fixide deposite account, waziri hiyo massage sent and delivered,” alisema Rais Magufuli.
Alipoulizwa juu ya kusimamishwa mkurugenzi huyo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya alisema hadi jana jioni hakuwa na taarifa yoyote.
“Sina taarifa yoyote ya kusimamishwa mkurugenzi huyo, hapa ni mambo mengi sijasikia,”alisema Waziri Manyanya.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi