MAPATO YA MECHI YA SIMBA NA YANGA YASHIKILIWA
KAMPUNI
ya Selcom Tanzania Limited inashikilia zaidi ya Sh. Milioni 130 za
mapato ya mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga katika Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara Oktoba 1, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Hiyo ni baada ya kuondolewa kwa makato mengine yote muhimu kwenye mapato
ya jumla ya mchezo huo ulioingiza Sh. Milioni 320 Simba na Yanga
zikitoa sare ya 1-1.
Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE imezipata zinasema
kwamba, fedha hizo zimezuiwa kwa maelekezo ya Serikali kufuatia
uharibifu uliojitokeza katika mchezo huo wa Oktoba 1, mwaka huu
mashabiki wa Simba wakivunja viti.
Na
taarifa zinasema kwamba Serikali imezuia fedha hizo hadi hapo uchunguzi
utakapokamilika juu ya hasara iliyojitokeza, ambayo kimsingi Simba
wamekubali kulipa.
Habari zinasema mchezo huo uliingiza Sh. Milioni 320 wakati uharibifu uliofanywa na Simba unakaribia kuwa wa Sh Milioni 400.
Makato ambayo yamekwishaondolewa kwenye mapato hayo ni pamoja na
asilimia18 ya VAT, asilimia 15 ya gharama za Uwanja, asilima 9 ya Bodi
ya Ligi, asilimia 5 ya TFF, asilimia 3 ya DRFA na asilimia 8 ya gharama
za mchezo.
Wenyeji Yanga SC wanastahili kupewa asilimia 40 ya mapato hayo wakati asilimia 20 ni za waliokuwa wageni, Simba SC.
Tayari Simba SC wameandika barua TFF kuomba wapatiwe mgawo wao wa mchezo
huo kwa kuwa wanahitaki fedha za kujiendesha kwa wakati huu na deni
hilo watalipa taratibu.
Hatua hiyo inakuja kufuatia mashabiki wa Simba kufanya vurugu Uwanja wa
Taifa Oktoba 1, baada ya Yanga kupata bao la kuongoza dakika ya 26
lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin
Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Na
katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba
SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
Kwa hali hiyo, mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya
mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa
uwanjani. Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza
mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya
87 kwa bao la Shizza Kichuya. Lakini tayari TFF imeipiga Simba SC faini
ya Sh. Milioni 5 kwa kosa hilo.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi