ASKOFU MAKALA AAGWA RASMI BAADA YA KUSTAAFU

Na Isaac Masengwa!

Askofu wa kwanza wa KKKT Dayosisi Kusini Mashariki ya ziwa Victoria iliyopo mikoa ya Shinyanga na Simiyu, Mchungaji Daktari Emmanuel Joseph Makala aliyestaafu mwishoni mwa mwezi April, 2023 ameagwa rasmi na washarika wa dayosisi hiyo.

Tendo hilo la kumuaga limefanyika katika ibada ya Jumapili ya tarehe 23 Julai, 2023 katika Kanisa la KKKT - DKMZV Usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Shinyanga.

Ibada hiyo imeongozwa na Mkuu  wa Dayosisi hiyo Askofu Daktari Yohana Ernest Nzelu ambaye ni askofu wa pili wa dayosisi hiyo akishirikiana na maaskofu wengine waliofika kwa wingi kwenye ibada hiyo pamoja na mgeni Rasmi katika tendo hilo Mkuu wa mkoa wa Simiyu Daktari Yahaya Nawanda.

Akitoa neno la shukrani Askofu daktari Ernest Yohana Nzelu amempongeza na kumshukuru Askofu Makala kwa utumishi wake shambani mwa Bwana.

"Kwa niaba ya wanadayosisi wote tunakupongeza na kukushukuru kwa utumishi wako mwema uliotukuka. Tunatambua na kuthamini juhudi ulizozifanya za kulitumikia kanisa la Mungu katika Dayosisi yetu. Sisi hatuna cha kukulipa zaidi ya kusema asante ila tunajua Mungu aliye mbinguni atakulipa". Alisema Askofu Nzelu

Askofu Makala alichaguliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi hiyo Desemba 12, 2012 na kuingizwa kazini Mei 5, 2013 ibada iliyofanyika katika Kanisa la KKKT - DKMZV Usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu ikiongozwa na aliyekuwa mkuu wa KKKT kipindi hicho Askofu daktari Alex Gehaz Malasusa.

Akitoa itikio la kustaafu kwake Askofu Joseph Makala amesema ataendela kushirikiana na kanisa pamoja serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Mheshimiwa mgeni rasmi namshukuru sana Mungu kwa kunipa miaka 40 ya kulitumikia kanisa, pia nakushukuru wewe mgeni rasmi kwa kuja kwako katika ibada ya kustaafu kwangu, nami nakuahidi nitaendelea kushirikiana na kuiombea serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania"

"Pia nakushukuru sana baba Askofu Nzelu, wachungaji na washarika wote wa Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, mmekuwa pamoja nami katika utumishi wangu, isingekuwa rahisi kuitenda kazi hii bila ushirikiano wenu na Mungu awabariki sana!. Naahidi nitaendelea kushirikiana na kanisa kwa kadri Mungu atakavyonitumia". Alisema Askofu Makala.

Naye mgeni rasmi Mheshimiwa daktari Yahaya Nawanda ametoa salaam za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akimpongeza Askofu Makala kwa utumishi wake.

"Baba Askofu Makala Mheshimiwa Rais anakupongeza sana na anakutakia maisha mema yenye neema ndani yako. Serikali itaendelea kushirikiana na wewe pamoja na mrithi wa nafasi yako Askofu Ernest Nzelu katika kuendeleza huduma hii."

"Nakupongeza kwa kuamua kustaafu kwa hiari tena kwa amani na utulivu mkubwa, umeonesha mfano mzuri kwa walio chini yako. Viongozi wa kanisa na wa serikali ni vema tukajifunza kupitia hili. Ingewezekana kabisa kusababisha migogoro kwa kanisani kama tu ungeamua kung'ang'ania madarakani".

"Mafanikio yoyote ya taasisi hutokana na uongozi imara na hii baba Askofu umeonesha ni jinsi gani uongozi wako ulikuwa imara na kwa hakika tumeona umeliacha kanisa likiwa salama." Alisema Mheshimiwa Nawanda.

Pia amempongeza Askofu Makala kwa kuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili katika mkoa wa Simiyu na Shinyanga hasa kuwajali na kuwalea watu wenye ulemavu wa ngozi (ualibino)

"Nizidi kukupa pongezi kwa juhudi zako na kuwa mstari wa mbele katika harakati za kupinga ukatili hasa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (ualibino) hususan katika mkoa wa Simiyu,  uliweza kukutana na waganga wa kienyeji ukazungumza nao hata kucheza nao mpira ikiwa lengo ni kutafuta amani kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, Mungu akukumbuke kwa moyo wako wa huruma kwa watu hao"

"Kupitia tukio hili la leo inatufundisha kuwa kutumika kwa uaminifu kuna faida zake nyingi sana, hivyo na sisi tunakuahidi kufuata nyayo zako katika utumishi wetu hata sisi tuliopo serikalini." Alisema mgeni rasmi

Akihubiri katika ibada hiyo Askofu Kesho Mshahara wa KKKT Dayosisi ya Kagera Magharibi kupitia kichwa cha somo UCHAGUZI WA BUSARA amesema kuwa Askofu Makala amechagua uchaguzi wa Busara kustaafu nafasi yake hiyo kwa kufuata katiba iliyoweka na dayosisi hiyo.

"Busara ni zaidi ya kujua, zaidi ya ujuzi na ujuzi mzuri ni pale unapofanya uchaguzi wenye msaada. Mfano Dakitari anayejua madhara ya kuvuta sigara halafu naye bado anavuta sigara huyo uchaguzi wake sio wa Busara".

"Nampongeza sana Askofu Makala kwa kuchagua uchaguzi wa busara kustaafu kwa hiari yake mwenyewe. Kama asingechagua kwa busara si ajabu angetolewa madarakani kwa nguvu. Kwa hiyo alichokifanya Askofu Makala ni uchaguzi wa busara na amekuwa mwaminifu kwa Mungu hata kwa katiba ya Dayosisi". Alisema Kesho Mshahara

Pia ibada hiyo ilihudhuriwa na wageni mbali mbali ikiwa ni pamoja na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Christina Solomon Mndeme pamoja na maaskofu  mbalimbali wa KKKT na madhehebu mengine kutoka ndani na nje ya Tanzania

Naye mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi. Christina Solomon Mndeme amempongeza Askofu Makala kwa kulitumikia kanisa na Taifa kwa ujumla.

"Askofu Makala kwa niaba ya serikali ya mkoa wa Shinyanga, tunakupongeza sana kwa kazi yako njema ya kulijenga kanisa la Mungu, tunakushukuru sana"

Wewe kama makamu mwenyekiti wa kamati ya amani ya mkoa wetu, tutaendelea kushirikiana na wewe katika mambo yote mema ya kuleta amani katika mkoa wetu, pia tunakuomba uendelee kumuombea Rais wetu Mh. Samia Suluhu Hasan ili aendelee kuliongoza Taifa hili kwa amani" Alisema Mheshimiwa mkuu wa mkoa

"Napenda nikupe ujumbe neno kutoka katika kitabu cha Musa cha KUTOKA 15:2, na neno hili likawe mwangaza katika maisha yako yote Ameen!"

Post a Comment

Previous Post Next Post