
Kiungo na nahodha wa zamani wa Yanga Haruna Niyonzima amesema anaipa nafasi timu yake ya zamani kutetea ubingwa wa ligi kuu waliotwaa msimu uliopita
Niyonzima ambaye hivi karibuni alikuwa nchini na timu ya Taifa ya Rwanda kwa ajili ya kuwania mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya CHAN dhidi ya Ethiopia, amesema anaiona Yanga ikiwa bora zaidi kuliko wapinzani wake katika mbio za ubingwa baada ya usajili makini uliofanyika huku pia wakiwa na wachezaji wote waliokuwa nao msimu uliopita
"Nafikiri Yanga bado wako vizuri sana. Msimu uliopita walifanya mapinduzi kwa kuweka pesa na kusajili wachezaji bora ambao waliungana na kuwa kitu imara kisha kuipiku Simba"
"Msimu huu pia wamejipanga sana, wameweza kubakisha mastaa wao wote wa msimu uliopita na iuongeza wengine bora hivyo watasumbua sana na kwa nilivyoiona ligi hadi sasa ni ngumu kuizuia Yanga kuwa bingwa" alisema Niyonzima
Niyonzima aliitumikia Yanga kwa takribani misimu sita kabla ya kusajiliwa Simba aliyoitumikia misimu miwili na baadae kurejea tena Yanga kwa msimu mmoja
Kwa sasa Niyonzima anaichezea AS Kigali ya kwao Rwanda, amehusishwa kuhitajika na matajiri wa Singida Big Stars ambao hata hivyo inaonekana mpango wa kumsajili haukufanikiwa
Dirisha la usajili litafungwa Jumatano August 31, 2022
Tags:
michezo