BINTI wa miaka 17 (jina linahifadhiwa), amenusurika kifo alipokwenda kwa mganga wa jadi kujifungua baada ya siku zake kupitiliza na mganga huyo kutumia dawa za mitishamba kumnywesha ili kuongeza uchungu na zingine kumwingiza kwenye njia ya uzazi na mtoto kushindwa kutoka.
Binti huyo mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, alilazimika kukimbizwa kituo cha afya baada ya mganga huyo kushindwa kumzalisha na kutokomea kusikojulikana.
Pia imeelezwa kuwa mganga huyo alikuwa anaingiza dawa hizo kwenye njia ya uzazi zimsaidie kama ganzi.
Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto wa halmashauri hiyo, Caroline Maliseli, alibainisha hayo jana, wakati akizungumza na gazeti hili kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 18, mwaka huu, baada ya mama mzazi wa binti huyo kukiri kwamba alikosa fedha ya nauli ya kumpeleka binti yake zahanati kujifungua.
Alisema mwanawe alipitiliza muda wake wa kujifungua wa miezi tisa na kuamua kumpeleka kwa mganga wa jadi kujifungua kienyeji.
Alisema walipofika kwa mganga huyo walipewa dawa za miti shamba za kuongeza uchungu na nyingine kuingiziwa sehemu za siri hali iliyomsababisha maumivu makali.
Kadhalika, wakati wanaendelea kumweka dawa hizo, mtoto alikuwa ameshachungulia katika njia yake ya uzazi akiwa ametanguliza uso na mganga huyo anadaiwa kuendelea kumsokomeza dawa hizo kwa vidole vyake vilivyokuwa vikimchoma mtoto mdomoni, usoni na puani.
Caroline alisema, baada ya hali hiyo binti huyo alizidiwa kutokana na maumivu makali na uchungu kuongezeka uliosababishwa dawa za miti shamba alizokuwa akisokomezwa.
Alisema, binti alikimbizwa Zahanati ya Mpera na hali ilivyozidi kuwa mbaya walimpeleka Kituo cha Afya cha Mwendakulima kwa matibabu zaidi.
Alipofikishwa kituoni hapo walibaini njia yake ya kawaida ilikuwa ndogo na mtoto kushindwa kupita hali iliyolazimu kumfanyia upasuaji na kumnusuru yeye na mtoto wake.
Mtoto alipotolewa alikutwa amevimba mdomo na pua kutokana na kuchomwa na vidole vya mganga wakati akimsokomeza dawa mama yake.
“Hali ya binti inaendelea kuimarika, lakini mtoto wake hawezi kunyonya kwa sababu aliumia midomo yake, tunaendelea na matibabu na hali yake itakapoimarika tutamkabidhi mama yake ili amnyonyeshe…Niombe waganga wa kienyeji kuacha kuingilia fani ambazo haziwahusu,” alisisitiza Maliseli.
Mama mzazi wa binti huyo (jina linahifadhiwa), alisema mtoto wake alikuwa ameolewa Kijiji cha Mwajilingo, Nzega, mkoani Tabora na alipopata ujauzito na kukosa matunzo alikimbilia nyumbani kwake wakati huo alikuwa ameshapitiliza muda wa kujifungua.
Alisema, sababu ya kumpeleka kwa mganga huyo ni kukosa Sh. 15,000 na vitenge viwili.
Alidai kuwa hakujua madhara ya kumpeleka mwanawe kwenda kujifungua kwa mganga wa jadi na kuiomba serikali isimchukulie hatua.
Akiongea na Nipashe, binti huyo alisema anamshukuru Mungu amejifungua salama licha ya kufanyiwa upasuaji.
Ofisa Muuguzi wa Kituo cha Afya Mwendakulima, Christian Jackson alisema, alimpokea Maua akiwa katika hali mbaya na kama wangechelewa kumpatia huduma ya upasuaji angeweza kupoteza maisha yeye pamoja na mtoto wake tumboni.
Tags:
habari