
LIGI Kuu Bara msimu ujao itaanza Agosti 17 mwaka huu na kumalizika Mei 27, ila kuna uwezekano mkubwa wa Simba na Yanga kukutana kwenye Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 13, lakini itategemeana na matokeo ya Fainali ya Kombe la ASFC inayopigwa wikiendi hii. Kama Yanga itaifunga Coastal Union katika fainali hiyo ya Arusha basi Simba iliyomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu itaumana na Yanga, lakini kama Wagosi watashinda, Ngao ya Jamii itazikutanisha Yanga na Coastal.
Kanuni ya kucheza mechi ya Ngao ya Jamii inaeleza, bingwa wa ASFC atacheza na bingwa wa Ligi Kuu Bara ambao ni Yanga, lakini kama bingwa wa ligi ndiye huyo huyo bingwa wa ASFC basi mshindi wa pili wa ligi atakipiga na bingwa wa ligi.
Bodi ya Ligi (TPLB) juzi ilitangaza kalenda mpya ya msimu wa 2022-2023 kuonyesha baada ya Ngao ya Jamii inayoshikiliwa na Yanga iliyoifunga Simba mwanzoni mwa msimu ulioisha jana, mechi za Ligi Kuu zitanza kupigwa Agosti 17 hadi Mei 27 msimu utakapomalizika.
Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almas Kasongo alisema ligi itaanza huku usajili ukiwa unaendelea kwani unatarajiwa kufunguliwa rasmi Julai Mosi na kufungwa Agosti 30 mwaka huu.
Alisema ligi Ligi ya Championship yenyewe itaanza Septemba 17 na kumalizika Mei 13 mwakani huku First League ikitarajiwa kuanza Oktoba 15 na kumalizika April Mosi mwakani.
Alisema ligi kuu msimu ujao itaendelea kama kawaida hata wakati wa Fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Novemba mwaka huu.
TumeLAZIMIKA KUirudia habari hii baada ya MKANGANYIKO ULIOJITOKEZA KWENYE TOLEO LA JANA juu ya ufafanuzi mechi hiyo ya Ngao ya Jamii. tUNAOMBA RADHI KWA USUMBUFU ULIOTOKEA-Mhariri.
Tags:
michezo