Serikali ya mkoa wa Shinyanga imejipanga kuhakikisha inavutia wawekezaji katika nyanja ya elimu upande wa vyuo vikuu.
Hayo yamesemwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhani Masumbuko kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 10 ya Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto kinachomilikiwa na Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) yaliyofanyika siku ya Ijumaa Julai 29, 2022 katika ukumbi wa chuo hicho.
Masumbuko amekipongeza Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto kwa kutoa Programu mbalimbali na kuanza mchakato wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Kolandoto akisema ni mipango ya mkoa wa Shinyanga kuanzisha vyuo mbalimbali mkoani humo ili kuongeza fursa za kiuchumi.
“Serikali ya mkoa wa Shinyanga inaendelea kuvutia wawekezaji mbalimbali ili wawekeze katika vyuo ili kuubadilisha mkoa wa Shinyanga…Ni fursa kwenu kuchangamkia fursa ya elimu ya juu sisi mkoa tumejipanga kufanikisha haya”,amesema.
“Serikali imeridhia kutoa sehemu ya eneo la shule ya Msingi Kolandoto ili kuongeza eneo la chuo cha Kolandoto",amesema Masumbuko.
Aidha amewataka wahitimu hao kwenda kuzingatia maadili pindi watakapoanza kuhudumia wananchi katika jamii.
“Elimu hii mliyopata ni elimu kubwa na sasa mnaenda kuingia katika ulimwengu wa kiutendaji, mnapaswa kwenda kuwa chachu, mkawe waadilifu mnapohudumia wananchi, mavazi yenu yakawe mazuri, lugha nzuri, na mkajiendeleze kielimu pia, elimu za juu zitawapa fursa zaidi za ajira”,amesema Masumbuko.
Jumla ya wanafunzi 255 wametunukiwa Stashahada na Astashahada katika Programu za Uuguzi na Ukunga, Maabara ya Binadamu , Utabibu , Ufamasia na Ufundi ‘ Laboratory Assistant and Computer Application’.
Tags:
habari