WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI APIGWA KOFI NA MWANANCHI AKIWA KANISANI

Mwanamume mwenye umri wa miaka 39, anazuiliwa na Jeshi la polisi baada ya kukamatwa kwa madai ya kumpiga Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi nchini Uganda wakati ibada siku ya Jumapili, Juni 26. Waziri Musa Ecweru anadaiwa kulimwa kofi katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Michael, Uganda.

Waziri Musa Ecweru anadaiwa kulimwa kofi moto na jamaa huyo katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Michael, Kaunti Ndogo ya Wera katika Wilaya ya Amuria. Inaripotiwa kuwa waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kaunti ya Amuria, alikuwa amehudhuria misa katika kanisa hilo wakati Michael Okurut alipomvamia. Waziri huyo alikuwa amekwenda kupeleka trekta iliyokabidhiwa kwa Parokia ya Kikatoliki ya Wera na Wizara ya Kilimo.

Duru zilizoshuhudia tukio hilo zilidokeza Daily Monitor kuwa Okurut aliingia ndani ya jengo la kanisa kimya kimya na kwa upole na kuelekea madhabahuni. Kisha alipiga ishara ya msalaba kabla ya kumsogelea waziri huyo ambaye alikuwa akiwahutubia waumini na kumpiga kofi sikioni na kuwaduwaza washirika. “Alikuja kimya kimya na hata kufanya ishara ya msalaba. Nilifikiri angejitafutia kiti kama walivyokuwa wakifanya washiriki wengine wa kutaniko lakini badala yake alienda kwa waziri na kunong’ona kabla hajampiga waziri kofi zito sikioni,” alisema mmoja wa mashahidi ambaye jina lake lilibanwa.

"Alijaribu kumpiga waziri kofi kwa mara ya pili lakini akazuia mkono wake kabla ya walinzi wake waliokuwa wakimsubiri nje kuingia kanisani na kumkabili (Okuru)," aliongeza.

Akithibitisha kisa hicho, Oscar Ageca ambaye ni kaimu msemaji wa polisi wa Kyoga Mashariki alisema Okurut alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Wera kuhojiwa. "Kesi ya shambulio ilifunguliwa katika kituo cha Polisi cha Wera ambapo taarifa zilinakiliwa na mshukiwa anazuiliwa huku mahojiano na uchunguzi wa kisa hicho ukiharakishwa," Ageca alisema. Akizungumza kuhusu kisa hicho, Waziri Ecweru alimtaja mshukiwa kuwa mgonjwa wa akili.

"Tumegundua habari zake za asili. Tumethibitisha kuwa alikuwa mwendawazimu. Wazimu wake humshambulia mara kwa mara na anapoteseka huwa mkali na mwenye jeuri,” Ecweru alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post