WANAFUNZI wa shule ya msingi Peaceland English Medium iliyopo Ukerewe Jijini Mwanza wamesema kuwa kitendo cha serikali kupitisha elimu bure kuanzia shule ya awali mpaka kidato cha sita itasaidia kuongeza watoto wengi kuendelea na masomo. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Mercy Lupimo ambaye ni mwanafunzi katika shule hiyo ameyasema hayo muda mfupi baada ya kutoka kwenye ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo wanafunzi hao walifanya ziara ya utembelea bunge nakujifunza shughuli za Bunge.
Lupimo amesema kuwa wanafunzi wataweza kuendelea na masomo kwa urahisi kwani wengi walishidwa kuendelea na masomo kutokana wazazi kuwa na kipato kidogo.
Mwanafunzi huyo ambaye pia ni dada mkuu katika shule hiyo amesema kuwa licha ya kuwa wanafunzi wataendelea na masomo pia ufaulu utaongezeka.
Sambamba na hilo amesema kuwa shule hiyo inapongeza serikali pamoja na bunge kwa kuona umuhimu wa wanafunzi ambao wanapewa ujauzito kurudi shuleni pindi wanapojifungua.
“Wapo wanafunzi wa kike ambao kwa bahati mbaya walikatiza masomo yao kwa kupata mimba .
“Watoto wa kike wanakumbana na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kumsababishia kupata mimba na hasa familia inapokuwa mbali na mtoto huyo au kushindwa kumpatia mahitaji muhimi,” ameeleza Lupimo.
Kwa upande wake Deodatus Amos ambaye ni mwanafunzi wa shule hiyo amesema kuwa kitendo cha kulitembelea Bunge wamepata kujifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kujua namna mihimili inavyoweza kufanya kazi bila kuingiliana.
“Tumetoka Ukerewe Mwanza kwa lengo la kilitembelea Bunge na tumeweza kujifunza mambo mengi hivyo tunawaomba wabunge kuwa watu wa kutenda hati pamoja na kuwatetea wananchi kwa ajili ya maendeleo” amesema Amos.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu msaidizi, David Onyango amesema kuwa shule hiyo ni shule ambayo inafanya vizuri kimasomo na mwaka 2019 ilishika nafasi ya kwanza kitaifa.
Hata hivyo amesema uzuri wa shule si kuwa na watoto wenye ufaulu tu bali ni pamoja na kuwa na wanafunzi wenye kuwa na nidhamu,utii pamoja na kujitambua.
Tags:
habari