CHAMA KILA KITU, AGUSIA MKWANJA WA YANGA



STAA wa Zambia, Clatous Chama amekiri kusikia tetesi zinazoendelea nchini Tanzania juu yake lakini akalitamkia Mwanaspoti kauli moja; “Muda utaongea.” Chama ambaye kwa sasa anakipiga na Berkane ya Morocco, aliuzwa huko na Simba mapema mwezi Agosti kwa zaidi ya Sh700Milioni.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Simba na Yanga zote kwa nyakati tofauti zimefanya mawasiliano na wakala wa mchezaji huyo na kila mmoja ametoa dau lake na lolote linaweza kutokea muda wowote kabla pilau ya Krismasi halijaliwa.

Chama kwa mara ya kwanza tangu kuondoka nchini amezungumza na Mwanaspoti live na kusema anajua na kusikia kila kinachoendelea kuhusiana na yeye kuhusishwa na kurejea nchini kwenye dirisha dogo la Krismasi.

Alisema kwamba hawezi kuingia kiundani juu ya suala hilo lakini muda utaongea. Staa huyo kipenzi cha mashabiki wa Simba amefafanua kwamba wakati mwingine huogopa kuzungumzia tetesi kwavile tafsiri huwa za namna mbalimbali. Alisisitiza kwamba kwa sasa kipaumbele chake ni familia yake kuhakikisha inakaa sawa, licha ya kutotaka kuingia kiundani zaidi katika ishu hiyo. Mkewe alifariki mwezi Juni mwaka huu na kumuachia watoto wadogo.

“Nakueleza ukweli na siwezi kuficha ukweli wa jambo hili au lingine lolote ila kila kitu kinakwenda vizuri na muda sahihi ukifika kila kitu kitakuwa wazi,” alisema Chama na kuongeza;

Mwanaspoti linajua kwamba Simba na Yanga kila mmoja amezungumza na staa huyo na wamemuahidi dau nono ingawa mpaka sasa hajafanya uamuzi wa mwisho.

Post a Comment

Previous Post Next Post