MABINGWA wa kihistoria wa soka nchini Tanzania, Yanga ya jijini Dar es Salaam imeipiga bao Simba kwa kuingiza mashabiki wengi viwanjani pamoja na kujikusanyia mapato ya mlangoni. Anaripoti Junior Mitanga, TUDARCo … (endelea).
Takwimu hizo za msimu wa 2020/21, zimetolewa leo Jumatano, tarehe 22 Septemba 2021 na Bodi ya Ligi Tanzania Bara zikionesha timu za Transit Camp ikishika mkia kwenye kuingiza mashabiki wengi na kujipatia mapato kiduchu.
Msimu huo wa 2020/21, ulimalizika kwa Simba kutetea ubingwa wake mara nne mfululizo na kutetea pia ubingwa wa kombe la shirikisho.
Licha ya Yanga kutoambulia kombe lolote, lakini ilijikusanyia mapato ya mlangoni ya Sh.986.82 milioni huku Simba ikishika nafasi ya pili kwa kupata Sh.929.7 milioni. Simba na Yanga zilitumia Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru.
JKT Tanzania iliyokuwa inatumia Uwanja wa Jamhuri Dodoma imeshika nafasi ya tatu kwa kupata Sh.148.14 milioni, Dodoma Jiji Sh.139.3 milioni ambayo nayo inatumia uwanja huo huku Azam FC yenye makazi yake Chamanzi, Dar es Salaam ikishika nafasi ya 15 kati ya 20 kwa kujikusanyia mapato ya Sh.72.69 milioni.
Katika timu zilizoingiza mashabiki wengi zaidi kwenye viwanja vya nyumbani msimu wa 2020/21, Yanga imeongoza kwa kuingiza mashabiki 141,681 ikifuatiliwana watani zao Simba ikiwa na mashabiki 138,518.
Azam FC imeshika nafasi ya 17 kati ya timu 20 ikiwaimeingiza mashabiki 11,465.
Tags:
michezo