
Suala la barua ya Serikali kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) likitakiwa ndani ya siku 10 kufuta waraka wake wa Pasaka uliotolewa Machi 24 limezua mjadala ndani na nje ya Bunge.
Waraka huo ambao mbali ya masuala ya kiroho, ulitaja changamoto tatu za kijamii, ulisababisha maaskofu wa dayosisi tatu kutengwa na Baraza la Maaskofu kwa kutotekeleza maelekezo ya kuusoma kwa waumini wakati wa ibada.
Wakati baadhi ya watu wakikosoa uamuzi wa KKKT kutakiwa kufuta waraka huo ndani ya siku 10 kuanzia Mei 30, wengi wakifanya hivyo kupitia mitandao ya kijamii; suala hilo limeibuliwa bungeni ambako pia imeelezwa barua nyingine imeandikwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Februari mwaka huu, TEC ilitoa ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2018 ndani yake ukieleza msimamo wa maaskofu 35 ambao mbali ya masuala ya kiroho pia ulizungumzia juu ya hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Hata hivyo, Mwananchi haijaona barua iliyoandikwa kwa TEC, huku katibu mkuu wa baraza hilo, Padri Raymond Saba akisema hawezi kuzungumzia suala hilo.
“Kwa sasa nipo kikaoni naomba uniache ila ukifika wakati nitalizungumzia,” alisema.
Alipotafutwa jana, Rais wa TEC, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alisema, “Siwezi kukubali au kukataa kwamba tumepokea barua hiyo ila wakati muafaka ukifika tutalizungumzia suala hilo.”
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alipoulizwa jana katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma kuhusu barua kwa KKKT na TEC alisema kwa kifupi: “Tutaitolea ufafanuzi baadaye.”
Juzi, katibu mkuu wa KKKT, Brighton Kilewa alithibitisha kupokea barua ya Msajili wa Vyama katika Wizara ya Mambo ya Ndani na kueleza kuwa baadhi ya maagizo yalishafanyiwa kazi.
Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson jana alizuia swali kuhusu barua hizo lisijibiwe na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Dk Tulia wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu alizuia swali la Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia kuhusu barua hizo kujibiwa.
Mbatia katika swali lake alisema kuna barua wamepewa KKKT na TEC wakitakiwa kufuta nyaraka zao, hivyo kutaka Waziri Mkuu aeleze uamuzi huo wa Serikali una lengo gani.
Baada ya swali hilo, Dk Tulia alisema, “Mtakumbuka Mheshimiwa (Saed) Kubenea (Mbunge wa Ubungo-Chadema) alimuuliza Waziri Mkuu swali linalohusu dini na Mheshimiwa Spika, alizuia swali hilo lisijibiwe.”
Kwa maelezo hayo, Dk Tulia alimwita mbunge mwingine kuuliza swali, huku Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi akinong’ona na wabunge wengine wa upinzani.
Baada ya kikao cha Bunge kuahirishwa jana asubuhi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliitisha kikao na waandishi wa habari ikiitaka KKKT na TEC kutojibu barua ya Serikali. Pia, waliitaka Serikali kuwaomba radhi waumini wa madhehebu hayo.
Wabunge hao walisema kuanzia sasa watahakikisha wanatumia mbinu mbalimbali ndani ya Bunge kuitaka Serikali kutoa majibu ya kina kuhusu barua hizo na hasa kuifuta barua yake.
“Wasijibu halafu waone Serikali itachukua hatua gani. viongozi hawa wa dini ni Watanzania na wana haki ya kutoa maoni, Serikali inapaswa kuwaomba radhi waumini,” alisema Mbatia.
Kaimu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Abdallah Mtolea alisema wameamua kuyasema hayo kwa kuwa yanayofanyika yanaweza kuivuruga nchi.
Mtolea ambaye ni Mbunge wa Temeke (CUF) alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika jamii hivyo Serikali iache kuingilia taasisi hizo.
Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika alisema, “Jambo hili haliwezi kuishia leo, katika siku 10 ambazo Serikali imezitoa sisi wabunge wa upinzani kila siku tukipata fursa bungeni tutauliza, tutahoji na tutatumia kanuni zote za Bunge kuitaka Serikali kutoa majibu na katika hili tutalifanya kwa umoja wetu.”
Maoni mtandaoni
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema: “Tishio la Serikali kwa Kanisa la KKKT linapaswa kupingwa na kila Mtanzania. Tukiruhusu KKKT kuingiliwa, hakuna atakayepona.”
Zitto pia ‘alitwiti’ kwenda kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akisema: “Nimeambiwa kuwa TEC pia imepewa barua kama ya KKKT. Serikali ya CCM imeamua kupambana na makanisa mawili makuu nchini ...”
Kwa ujumbe huo, Polepole alijibu: “Serikali makini ina wajibu wa kukumbusha, kuelekeza, kuonya au kuchukua hatua kwa mtu/taasisi yoyote inayokwenda kinyume cha taratibu za nchi ambazo tumejiwekea. Nimeisoma barua ya Msajili anazo hoja za msingi. Usijichomeke hapa kutafuta huruma na umaarufu hewa. Soma Warumi 13:1-5.”
Barua ya Msajili wa Vyama ya Mei 30, iliyotiwa saini na M. L. Komba kwa niaba ya msajili iliyosambaa juzi kwenye mitandao ya kijamii ikielekezwa kwa mwenyekiti au askofu mkuu wa KKKT inaeleza taasisi hiyo imeshindwa kutekeleza masharti ya usajili kwa kushindwa kulipa ada za mwaka, kutoa taarifa za mikutano, fedha na mabadiliko mbalimbali, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ameandika: “Serikali inawalazimisha KKKT waombe ridhaa serikalini ili waruhusiwe kubadilisha katiba yao. Serikali hiyohiyo, inaongoza nchi kwa katiba iliyochoka na isiyoendana na mahitaji ya sasa. Tunawataka @TZMsemajiMkuu kwanza mbadilishe Katiba ya JMT kabla hamjagusa ile ya KKKT.”
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji ameandika: “Nimeona barua hii kwa masikitiko na majonzi makubwa. Naweza sema tu kwamba, “Hakuna mtu mwenye akili timamu aliyewahi kuvunja kioo kilichomwonyesha uchafu wake.”
Mwananchi ilitafuta maoni ya wachungaji wa kanisa hilo na mmoja aliyejitokeza, Christosiler Kalata alisema KKKT haina baraza la maaskofu, bali mkuu wa kanisa, akiwa kiongozi wa wajumbe wa halmashauri, kamati na bodi za kanisa.
Alisema katibu mkuu wa kanisa ndiye anayeagizwa kupeleka taarifa za kanisa kwa jamii.
“Suala la kanisa kufuta waraka wake ni mwendelezo wa mawasiliano ambayo yanatakiwa kurudishwa katika maadili yetu ambayo tumekuwa nayo katika utamaduni wetu,” alisema.
Mchungaji Kalata alisema, “Kusema kwamba baraza la maaskofu halina uwezo wa kisheria, kama nilivyosema hapo juu, mkuu wa Kanisa anayo mamlaka ya Kimungu, unaposema kisheria unagusa mamlaka nyingine ambayo ni ya kiserikali, hakuna askofu anayelishwa maneno ya kutamka yanayotoka kwa Mungu, akitamka kinyume cha alivyotumwa na Mungu, Mungu anamshughulikia papo hapo! Akijiingiza upande mwingine akatamka maneno yenye upungufu na kuleta sintofahamu kwa jamii, mamlaka zinazohusika haziwezi kumwacha.”
Alisema, “Katika hali ilivyo tumeona hata ndani ya kanisa tukifanya makosa, serikalini wakifanya makosa, wakati fulani kila mtu anakosea. Na kabla ya kuwahukumu wengine, afadhali watu watambue kwamba labda siku moja wao wenyewe walikosa katika jambo lilelile! Mungu anaalika kuhojiana, tena ana kwa ana bila shaka Mungu anaturejesha katika mstari huo,” alisema Mchungaji Kalata.
Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Tausi Mbowe, Bakari Kiango na Elizabeth Edward.
Tags:
habari