SINGIDA YAAHIDI KUILIZA TENA YANGA TAIFA LEO

Singida United imejigamba kuwatoa nishai tena Yanga kwa kuifunga katika mchezo wa ligi kuu utakaofanyika uwanja wa Taifa leo saa 10 jioni.

Aprili mosi mwaka huu Singida iliwatoa Yanga katika mchezo wa kombe la FA kwa mikwaju ya penati 4-2 mtanange uliopigwa uwanja wa Namfua mkoani Singida.

Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo, Festo Sanga amesema wanaiheshimu Yanga kwakua ni mabingwa watetezi lakini maandalizi waliyofanya wanaamini wataondoka na alama zote tatu.

Singida imetoka kupoteza mchezo nyumbani kwa kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar wiki iliyopita.

"Tuna kila sababu ya kuifunga Yanga leo, tumefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huu na wachezaji wapo katika hali nzuri ya kuibuka na ushindi," alisema Sanga.

Yanga na Singida zimekutana mara tatu kila timu ikishinda moja na kwenda sare moja na leo itakuwa ya nne kukutana.

Post a Comment

Previous Post Next Post