YANGA SI YA MCHEZOMCHEZO...NI MOTO WA KUOTEA MBALIMBALI


YANGA ni moto na haizuiliki baada ya mabingwa hao wa soka nchini jana Jumapili kuizima Majimaji Songea iliyokuwa uwanja wake wa nyumbani wa Majimaji mjini hapa kwa mabao 2-1 na kutinga kwa kishindo robo fainali ya michuano ya Kombe la FA.

Mabao mawili matamu ya vichwa ya Pius Buswita na Emmanuel Martin katika kila kipindi, yaliiwezesha Yanga kuzifuata Njombe Mji, Singida United, Azam na Mtibwa Sugar zilizotangulia mapema kutinga hatua hiyo, huku ikiwapa burudani mashabiki waliofurika kwa wingi uwanjani hapo.

Pambano hilo lililokuwa kali na lenye ushindani kwa muda wote wa dakika 90, lilihudhuriwa na umati mkubwa wa mashabiki huku wenyeji wakipigwa tafu na manazi wa Simba waliokuwa wakiishangilia mwanzo mwisho kabla ya kunyamazishwa.

Wachezaji wa Majimaji ambao awali walifanya mgomo baridi ili kushinikiza kulipwa fedha zao za usajili na mishahara kiasi cha kuwaweka roho juu mashabiki wao, walilianza pambano hilo kwa kasi na kuwatia hofu mashabiki wa Yanga.

Hata hivyo Yanga ikicheza kwa tahadhari kubwa kutokana na rekodi mbaya waliyonayo kwenye uwanja huo wa Majimaji ilitulia na kuwabana wenyeji wao kabla ya kuandika bao la kuongoza katika dakika ya 40 baada ya Buswita kuupiga kiufundi kwa kichwa mpira mrefu wa beki Haji Mwinyi mbele ya lango la Majimaji.

Kabla ya kupiga krosi hiyo, Mwinyi alipokea pasi murua ya kiungo Papy Kabamba Tshishimbi aliyeendelea kuonyesha umuhimu wake katika kikosi cha Wana Jangwani.

Bao hilo lilidumu hadi mapumziko, licha ya Majimaji kucharuka kutaka kulirejesha.

Katika kipindi hicho cha kwanza Yanga ilitengeneza nafasi chache kulinganisha na wenyeji wao ambao washambuliaji wake, Marcel Bonventure, Peter Mapunda na Jaffar Mohammed walitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia hasa kwa kunaswa kila mara na mtego wa kuotea waliotegewa na mabeki wa Yanga.

Katika kipindi cha pili Yanga ilianza kwa moto mkali na kuwakimbiza Majimaji kabla ya kuandika bao la pili lililofungwa na Martin katika dakika ya 57 akimalizia kwa kichwa krosi tamu ya Hassan Kessy aliyeng’ara katika pambano hilo.

Kabla ya kupiga krosi hiyo iliyotokana na pasi murua ya kisigino ya Buswita, Kessy alimgeuza atakavyo beki Mpoki Mwakinyuki na kumimina majalo iliyokwamisha wavuni na Martin na kuwafanya Uwanja wa Majimaji kulipuka kwa hoihoi.

Hata hivyo Majimaji hawakukatishwa tamaa na bao hilo la pili na kuendelea kufanya mashambulizi makali na hatimaye dakika nne baadaye waliandika bao la kufutia machozi lililofungwa kwa kichwa na Jaffar Mohammed akiunganisha krosi ya Aziz Sibo.

FULU KUJIAMINI

Yanga iliingia Songea juzi Jumamosi ikiwa inajiamini kupita kiasi na hata jana waliwahi mapema kuibuka uwanjani saa 8:30 mchana na kuwafanya mashabiki waliowahi Majimaji kuwashangilia mwanzo mwisho na kuwapa faraja kubwa nyota wa timu hiyo.

Hata hivyo mashabiki wa Yanga waliojazana uwanjani hapo walipata wakati mgumu kutoka kwa wenzao wa Majimaji walioungwa mkono na wale wa Simba waliokuwa na jezi za klabu ya Msimbazi zenye rangi nyekundu na nyeupe.

Mchezo ulipoanza, Yanga ilianza kwa kasi na katika kipindi hicho cha kwanza ilipata kona tano dhidi ya mbili za wenyeji wao, lakini zote hazikuwa na madhara mpaka dakika 40 Buswita alipobadilisha upepo na kuwapa furaha mashabiki wa Yanga.

Katika kipindi hicho timu zote zilifanya mabadiliko, Yanga ikiwatoa Martin na Rafael Daud na kuwaingiza Julius Mhilu na Geofrey Mwashiuya, huku Majimaji ikimtoa Jaffar na nafasi yake kuchukuliwa na Paul Lwanga.

Vikosi:

YANGA: Rostand, Kessy, Mwinyi, Makapu, Yondani, Pato, Rafael. Mhilu, Tshishimbi, Ajibu, Buswita, Martin/Mwashiuya.

MAJIMAJI: Malande, Sibo, Mpoki, Salamba, Mohammed, Kikoti, Hamis, Kibiga, Mapunda, Bonventure, Jaffar/Lwanga.

MTIBWA SUGAR YAPENYA

Katika mechi nyingine ya mapema mchana iliyopigwa Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza, Mtibwa Sugar waliizima Buseresere ya Geita inayoshiriki Ligi ya Mkoa kwa kuitungua mabao 3-0 yote yakipatikana kipindi cha pili.

Mabao hayo yalifungwa na Hassan Dilunga kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 52 kabla ya Haruna Chanongo kuongeza la pili dakika ya 83 na Ally Makarani kumaliza udhia sekunde chache kabla ya mchezo huo kumalizika.

Michuano hiyo itahitimisha mechi za Raundi ya 4 leo Jumatatu kwa michezo miwili ambapo mapema mchana Kiluvya United ikiwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Mabatini, Mlandizi, Pwani itaikaribisha Prisons Mbeya na jioni, Stand United ikiwa Kambarage Shinyanga itaialika Dodoma FC inayonolewa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

Post a Comment

Previous Post Next Post