OKWI AFICHUA SIRI ZA SIMBA KUPATA USHINDI KILA WANAPOSHUKA DIMBANI

Mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Mghana Emmanuel Okwi amesema kikosi chao kinajizatiti kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC na baadaye wataelekeza nguvu kwa wapinzani wao wa Kombe la Shirikisho Afrika, timu ya Al Masry ya Misri.

Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba Sc, watawakaribisha Mbao Fc, katika mchezo wa ligi hiyo utakaofanyika Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Okwi alisema kuwa kila siku wanajiandaa na kujiimarisha kwa kuzingatia mchezo unaofuata na hiyo ndiyo mbinu sahihi ya kuhakikisha wanapata pointi tatu kila wanaposhuka dimbani.

Okwi alisema kuwa wataikabili Mbao FC bila kujali matokeo ya sare ya mabao 2-2 waliyopata kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza, kwa sababu kila timu inaingia tofauti katika hatua ya lala salama ambayo bingwa na klabu zinazoshuka daraja hujulikana.

"Najua wengi wanaiwaza mechi dhidi ya Al Masry, lakini kumbukeni tunamechi nyingine dhidi ya Mbao kutoka Mwanza, ni mchezo mgumu ambao tunatakiwa kupambana ili tupate pointi tatu na kujiweka katika mazingira bora ya mbio za kuwania ubingwa," Okwi alisema.

Mshambuliaji huyo aliongeza kuwa bado katika mawazo yake hakufikiria kuwaza kuwania kiatu cha dhahabu lakini anafurahi kuona Simba iko kileleni na yeye ndiye anaongoza kwenye safu ya washambuliaji msimu huu.

"Sikupanga kuwania kiatu cha dhahabu, awali malengo yangu yalikuwa ni kuisaidia timu ili kutwaa ubingwa, lakini sasa niko kwenye nafasi hiyo, hivyo naongeza nguvu kuhakikisha pia napata tuzo hiyo kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu," aliongeza Okwi.

Naye Afisa Habari wa Simba Haji Manara, alisema kuwa wanawaomba mashabiki wa timu hiyo kuendeleza umoja ili waweze kutimiza malengo yao katika mechi zilizobakia za nyumbani na ugenini.

Baada ya mechi hiyo dhidi ya Mbao FC, Simba itaendelea kukaa Jijini Dar es salaam kuwasubiri Stand United kutoka Shinyanga na Machi 09 mwaka huu itawakaribisha Al Masry katika mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Chanzao-nijuzehabari

Post a Comment

Previous Post Next Post