
Okwi ambaye hajawahi kutwaa tuzo ya ufungaji bora nchini tayari ameivunja rekodi yake ya mabao 12 aliyoweka 2011-12, kwa kufunga magoli hayo mawili yanayomfanya kufikisha mabao 16 msimu huu.
Katika mchezo Okwi alifunga bao lake la kwanza dakika 41 kwa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Mbao, David Mwasa.
Mganda huyo alifunga goli lake la 16 msimu huu dakika 71, kwa shuti kali la mguu wa kushoto lilokwenda moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa wa Mbao, Iyvan Rugumandiye asijue la kufanya.
Okwi msimu huu amekuwa na wastani wa kufunga bao 1.2 kwa kila mechi aliyocheza na endapo ataendelea kwa kasi hiyo katika michezo 11 iliyobaki basi anaweza kufikia au kuivunja rekodi ya mshambuliaji wa Yanga, Amiss Tambwe ya kufunga mabao 21, katika msimu 2015-16 ikiwa ni mabao mengi zaidi kufungwa kwa msimu mmoja katika kipindi cha miaka 12 iliyopita.
Katika msimu huu Tambwe aliingoza Yanga kutwaa ubingwa alifuatiwa Mganda Hamis Kiiza wa Simba aliyefunga mabao mabao 19, Mzimbabwe Donald Ngoma wa Yanga (17) na mshambuliaji wa Prisons,Jeremiah Juma (16).
Uwezo mkubwa alionyesha Okwi katika kufunga msimu huu hasa baada ya kuvunja mwiko wa kutofunga nje ya Dar es Salaam unampa nafasi kubwa ya kutwaa kiatu cha dhahabu.
Mganda huyo anatakiwa kufunga mabao sita tu katika michezo 12 iliyobaki ya Simba ili kufikisha magoli 20,sawa na rekodi iliyowekwa na mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma mwaka 2006 alipotwaa tuzo ya ufungaji bora.
Katika michezo 12 iliyobaki ya Simba saba atacheza kwenye Uwanja wa Taifa au Uhuru, Dar es Salaam viwanja ambavyo Okwi amefunga mabao yake 13 msimu huu.
Hivyo rekodi hiyo ya Okwi kwenye viwanja hivyo Dar es Salaam itawalazimu washindani wake wa kubwa katika kuwania tuzo ya ufungaji bora, Obrey Chirwa wa Yanga mwenye mabao 11 na John Bocco wa Simba mabao 10 kufanya kazi ya ziada.
Okwi alisema anachoangalia ni kuipa matokeo timu yake kwanza na ufungaji bora utakuja tu.
"Hakuna ambaye hapendi tuzo lakini muhimu kwanza kwa sasa ni kuisaidida timu yangu kushinda mechi zake zote.
"Ingawa kama itatokea nikamaliza mfungaji bora nitashukuru kwani kila mchezaji anapenda mafanikio lakini itapendeza zaidi kama tutatwaa ubingwa na nikaibuka mfungaji bora,"alisema Okwi.
Tags:
michezo