MAMBO 10 USIYOYAFAHAMU KUHUSU TIDO MHANDO

1. Tido Mhando ni mmoja wa watangazaji mahiri na wakongwe Tanzania imewahi kuwa nao. Ana uzoefu mkubwa katika tasinia ya habari na tayari amefanya kazi na vituo vya redio na runinga vya kitaifa na kimataifa kwa zaidi ya miaka 40.

2. Tido alianza kufanyakazi katika redio ya taifa, Radio Tanzania Dar Es Salaam (RTD) sasa hivi ni Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) akiwa mcheza muziki (DJ). Baada ya muda alijizolea umaarufu kwa kuwa mchambuzi bora wa mpira na pia mtangazaji aliyependwa.

3. Mwaka 1985 akiwa nchini Kenya, Tido Mhando alijiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akiwa mhabarishaji wa kwanza nchini humo.

4. Tido Mhando alihamishia makazi yake nchini Uingereza mwaka 1991 ambapo alikwenda kufanya kazi katika Makao Makuu ya Redio ya Kimataifa ya BBC.

5. Kwa miaka yote akifanya kazi na BBC, Tido alijipatia heshima kubwa kutokana na uwezo wake wa kutoa habari kuhusu nchi zinazozungumza lugha ya Kiswahili zikiwemo Ethiopia, Kenya, Somalia, Tanzania na Uganda.

6. Tido Mhando ni miongoni mwa wanahabari wachache waliopata nafasi ya kufanya mahojiano na marais walipo madarakani au marais wasataafu katika nchi za Afrika Mashariki na Kati. Miongoni mwa wengi, Tido amepata nafasi ya kuwahoji Rais wa DR Congo, Joseph Kabila, Rais mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki (kabla hajawa Rais), Rais Mstaafu wa Kenya, Daniel Arap Moi, Rais Mstaafu wa Rwanda, Paster Bizimungu na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Wengine ni Dikteta wa Uganda, Idi Amin, Rais wa Uganda Yoweri Museveni. Aidha amewahoji pia marais wawili wa Zanzibar ambao ni Salmin Amour na Amani Karume.

7. Mwaka 1990, Tido alikuwa ndiye mwanahabari wa kwanza kutoa habari kuhusu kupotea na baadae kufariki kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Dr Robert Ouko. Lakini pia, mwaka 2001 alikuwa mwanahabari wa mwisho kufanya mahojiano na aliyekuwa Rais wa DR Congo, Laurent Kabila siku chache kabla ya kuuawa.

8. Tido Mhando amewahikufanya kazi na vituo mbalimbali vya habari dunia vikiwemo Deutsche Welle (Ujerumani), Sauti ya America (VOA), Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) likijulikana kama Sauti ya Kenya (VoK).

9. Mbali na kuwa mwanahabari, Tido ameshika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika vyombo vya habari zikiwemo, Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kati ya 1999 mpaka 2006, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kati ya mwaka 2006 na 2010 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanspoti na The Citizen kuanzia 2012-2014. Kwa sasa Tido Mhando ni Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media Ltd.

10. Januari, 26, 2018 Tido Mhando alipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka matano. Mashtaka manne kati ya hayo ni ya matumizi mabaya ya madaraka wakati akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa TBC, na shtaka moja ni la kuisababishia serikali hasara ya TZS 887.1 milioni.

chanzo-swahilitimes

Post a Comment

Previous Post Next Post