KIMENUKA!! YANGA YAWAWEKEA MASHARTI MAGUMU WACHEZAJI HAWA

YANGA imemaliza uvumi wa kurudi kwa beki wake wa zamani, Vincent Bossou kwa kumsainisha Mkongomani Fistoo Kayembe huku Kocha George Lwandamina akiweka masharti magumu kwa wachezaji wote wapya wanaosajiliwa klabuni hapo kuanzia sasa.

Kayembe, ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili juzi akitokea klabu ya Sanga Balenge ya DR Congo, amelamba dili hilo baada ya Lwandamina kujiridhisha na kiwango chake uwanjani.

Beki huyo amepewa mkataba mgumu ambao, mara baada ya kumaliza miezi sita ya awali atalazimika kurudi mezani na uongozi wa Yanga kuangalia kiwango chake na kama miyeyusho anapigwa chini, kila kitu kimewekwa kwenye maandishi.

Lwandamina amelazimika kutumia akili hiyo kuwashauri mabosi wa Yanga baada ya kuchoshwa na tabia za baadhi ya wachezaji ambao, wakishasaini tu wanaanza mizinguo kama alivyo Donald Ngoma kwa sasa.

Kocha huyo amewaambia mabosi wa Yanga kuwa kuwekwa kwa vipengele hivyo muhimu vitamfanya kila mchezaji anayesajiliwa sasa kuwa makini katika kuitumikia klabu, lakini pia Yanga itaepuka hasara kwa kuvunja mikataba kwa wachezaji ambao wataonekana kutokuwa na tija klabuni.

“Nikweli nimeshauri hilo tunafanya hivyo, kwa lengo la kutaka kuona kila mchezaji anakuwa na jukumu la kuufanyia kazi mkataba wake. Haipendezi kuona mchezaji anasaini na baada ya hapo anakosa ushindani wa namba kwa kuchukua fedha bure. Nataka kuona klabu inapata kile inachokitarajia kwa mchezaji, lakini pia tunaepusha hasara ya fedha katika kuvunja mikataba, lakini kitu bora zaidi sasa tutaweza kuona kila mchezaji anajituma kutetea ajira yake,” anasisitiza.


Tunafahamu kuwa, aina hiyo ya mikataba itamuhusu pia mchezaji yoyote atakayesajiliwa kuanzia sasa akiwemo straika mpya anayesakwa na Yanga kutoka Guinea Bissau pamoja na kinda wa Serengeti Boys, Yohana Nkomola, aliyesaini tayari.

Kuhusu Ngoma, Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwassa alisema; “Mpaka tunavyoongea sasa sina taarifa yoyote ya kiofisi ikionyesha Ngoma alipewa ruhusa na klabu kurudi kwao au kwenda huko kwenye matibabu. Sasa alipewa ruhusa na nani ya kufanya hivyo ndio swali kubwa.



“Hii ni mara ya pili Ngoma anafanya kosa hili, na kuhusu adhabu zipo nyingi tunaweza kumkata mishahara yake, lakini kama haitoshi tunaweza kumpeleka katika kamati ya nidhamu kujadiliwa na huko ndio tutajua kuhusiana na hatma yake.”

Post a Comment

Previous Post Next Post