Waswahili wanasema ‘Mazoea hujenga tabia’ hicho kinachoendelea kwa Simba ilishindwa kutumia sare ya bao 1-1 ambayo Yanga waliipata dhidi ya Prisons ili iweze kuongeza pengo la pointi baada ya yenyewe kulazimishwa sare pia ya bao 1-1 na Lipuli FC.
Simba ambayo awali kabla ya mechi za mwishoni mwa wiki iliyopita ilikuwa mbele ya Yanga ambao ni washindani wake wakuu kwenye mbio za ubingwa kwa pointi mbili ikiwa na pointi 22, ingeongeza pengo la pointi kufikia nne kwani ingefikisha pointi 25 wakati Yanga ingebaki na pointi 21 ambazo imezifikisha baada ya kutoka sare na Prisons, Jumamosi iliyopita.
Hata hivyo rekodi za Ligi Kuu zinazoonyesha Simba wamekuwa wakipata wakati mgumu kupata matokeo mazuri katika idadi kubwa ya mechi za kutanua pengo la pointi baina yake na Yanga jambo ambalo mwishoni huwagharimu na kuwawezesha watani wao kutwaa ubingwa.
Mfano wa mechi hizo ni ile ya mwisho kwenye mzunguko wa kwanza msimu uliopita dhidi ya vibonde African Lyon ambapo walijikuta wakipoteza kwa bao 1-0 na kuwafanya washindwe kuongeza pengo la pointi dhidi yao na Yanga kufikia tano kwani walimaliza mzunguko huo wakiwa na pointi 35 huku Yanga wakiwa na 33.
Katika mzunguko wa pili msimu huo, Simba ilijikuta ikitoka sare mechi ya raundi ya 19 dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo ingeifanya iwe mbele ya Yanga kwa tofauti ya pointi nne.
Ikumbukwe katika msimu uliopita, Yanga ilitwaa ubingwa ikiwa pointi sawa na Simba lakini yenyewe ilinufaika kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa na pengine Simba ingezipata pointi katika mechi hizo, ingeweza kutwaa ubingwa.
Kitendo cha kutoka sare juzi dhidi ya Lipuli, kumeipunguzia mzigo Yanga ambayo imeendelea kuwa nyuma ya Simba kwa tofauti ya pointi mbili lakini kinaweza kuwa na faida kwa Azam FC ambayo inaweza kukaa kileleni iwapo ingefanikiwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo wake dhidi ya Mtibwa Sugar jana usiku.
Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma alisema tatizo hilo la Simba kushindwa kupata matokeo mazuri katika mechi ambazo wanapaswa kushind ili kuongeza pengo la pointi dhidi ya Yanga linatokana na athari za kisaikolojia.
"Unajua hizi ni timu kubwa hapa na hivyo ile presha wakati mwingine inawafanya wachezaji washindwe kutimiza kile kinachotarajiwa lakini pia wakati mwingine nadhani ni maandalizi ambayo wachezaji wanayapata kabla ya mechi husika.
“Inawezekana wachezaji huwa hawaandaliwi vizuri kwa ajili ya mechi za aina hii. Mfano kwenye mechi yetu dhidi ya Lipuli, tulianza vizuri kipindi cha kwanza lakini baada ya kupata bao, wachezaji walionyesha kuridhika na mwisho wa siku tumeshindwa kuibuka na ushindi," alisema kocha huyo.
Tags:
michezo