Simba vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa wakiwa na pointi 23, lakini kumbe nyuma yake kuna siri nzito. Washindi hao wa kombe la FA kumbe wamekuwa wakinunua kila pointi kwa Sh2.7 milioni kutokana na posho wanazotoa kwa kila mechi wanayoshinda.
Kama ulikuwa haujui mashabiki wa Simba kila mechi huwa wanachanga Sh5 milioni huku bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ naye akitoa Sh5 milioni na kuwakabidhi wachezaji endapo tu watashinda mchezo huo.
Kwa msimu huu, Simba imeshinda mechi sita hivyo kugharimu kiasi cha Sh60 milioni kama posho kwa wachezaji wake. Mkwanja huo hukabidhiwa kwa nahodha wa timu, Method Mwanjali mara tu mechi inapomalizika naye hugawa kwa wachezaji wenzake kwa kadri walivyokubaliana.
Simba hakuna maisha ya kutegeana kwani nyota wanaocheza hupata kiasi kikubwa tofauti na wale wanaokaa benchi. Kwa wale wanaoanza pamoja na walioingia baadaye hupata laki nne kila mmoja.
Wale ambao wapo katika benchi lakini hawakucheza kila mmoja anapewa laki tatu na wale ambao wamekaa jukwaani wanapata laki moja na nusu ikiwa ni kama shukrani kwa kufanya mazoezi na wenzao.
Mmoja wa wachezaji wa Simba, alisema; "Huwa naumia nikiona nashindwa kupata nafasi ya kucheza na najituma kila siku nikiwa mazoezini ili kupata nafasi ya kucheza kwani kiwango changu kitazidi kuimarika lakini katika mgawanyo huo wa pesa nitakuwa katika kundi linalopata pesa nzuri.”
Wakati Simba na Yanga wakiwa na utamaduni wa kugawa pesa papo kwa papo kila baada ya mechi kumalizika timu nyingine zimekuwa na utamaduni tofauti.
Azam wao wanatoa posho kwa wachezaji wao lakini huwa wanawapa mwisho wa mwezi kwa kuongeza katika mishahara yao.
Mtibwa na Kagera Sugar nao wana utamaduni kama wa Azam ambao mishahara na posho ya aina yoyote ile lazima itolewe mwisho wa mwezi kipindi ambacho mchezaji analipwa chake.
Tags:
michezo