SIKU moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
kutangaza vita dhidi ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, makubwa
zaidi yamezidi kujitokeza baada ya orodha ya watu hao wanaojihusisha na
biashara hiyo haramu kuongezeka.
Mkuu huyo wa mkoa amemuagiza Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Kamishna Simon Sirro kuwaongeza askari wengine watatu katika
orodha ya watuhumiwa hao ambao alidai katika wiki mbili zilizopita
walipewa Sh bilioni moja kutokana na biashara hiyo.
Aliwataja askari hao kuwa ni Muddy Zungu, Fadhili na Ben huku wengine
wanaopaswa kuongezwa katika orodha hiyo ni pamoja na msanii Vanesa Mdee
na Video Queen, Tunda Sebastian.
Aidha, Makonda alimuagiza Sirro kuhakikisha wasanii na watu wengine
walioko kwenye orodha aliyoitaja awali ambao hawakufika, wakamatwe mara
moja na wawekwe ndani hadi Jumatatu kwa ajili ya mahojiano.
“Hawa nataka waunganishwe na wale wenzao, hatuwezi kuwa na watumishi
wanaochafua taaswira ya jeshi la polisi na nimepata taarifa mmoja
amenunua nyumba Kigamboni,” alisema Makonda.
Makonda pia alimtaja mtu mwingine ambaye ni mfanyabiashara mkubwa wa
dawa hizo, Omari Sanga kuwa ni mmoja kati wa watu waliosababisha
asilimia 65 hadi 70 ya Watanzania waishie kwenye jela nchini China.
Pia aliitaja hoteli ya Meditteranian iliyopo Kawe kuwa nayo ni
miongoni mwa hoteli ambazo zimekuwa zikifanya biashara hiyo kinyume na
leseni waliyopewa.
Watuhumiwa waliofika ni pamoja na aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Wema
Sepetu, Khaleed Mohammed (TID), Hamidu Chambuso (Dogo Hamidu/ Nyandu
Tozzy) pamoja na Babuu wa Kitaa.
Imeandikwa na Katuma Masamba
HABARI LEO
Tags:
habari