TRA SHINYANGA YAWAHIMIZA WANANCHI NA WAFANYABIASHARA KUFANYA MAKADIRIO NA KULIPA KODI KWA WAKATI

 

 Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Bw. Emmanuel Maro 
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Shinyanga inawahimiza wafanyabiashara na wananchi wote kufanya makadirio ya kodi na kulipa kodi ya awamu ya kwanza kwa mwaka wa 2026 kabla au mnamo tarehe 31 Machi 2026. 

 Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Bw. Emmanuel Maro amesema kuwa kulipa kodi kwa wakati ni wajibu wa kila raia na ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa. 

Ameongeza kuwa kodi inayolipwa kwa wakati inasaidia Serikali kutoa huduma muhimu za kijamii, kiuchumi, na usalama kama vile ujenzi wa barabara, madaraja, shule, zahanati, huduma za afya, maji safi, na ulinzi wa wananchi.

“TRA tunawahimiza wafanyabiashara na wananchi kuhakikisha makadirio ya kodi yanafanywa mapema na kodi ya awamu ya kwanza inakuwa tayari kabla au mnamo tarehe 31 Machi 2026. Kulipa kodi kwa wakati hakusaidii tu kuepuka faini na riba, bali pia ni njia ya kushirikiana na Serikali katika kujenga Taifa letu,” amesema Bw. Maro.

Aidha, Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga amesisitiza kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kutoa risiti za kielektroniki kwa kila mauzo, huku wanunuzi wakihimizwa kudai risiti hizo ili kulinda haki zao na kuhakikisha uwazi wa mapato ya Taifa.

Bw. Maro amewataka wananchi wote kushirikiana na Serikali kwa kulipa kodi kwa wakati kwani kila shilingi inayolipwa ni mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwa maelezo zaidi:

Simu bure: 0800 750075 / 0800 780078

Barua pepe: huduma@tra.go.tz au services@tra.go.tz

Ukiukaji wa maadili: 0689 122 515 / 0689 122 516

Ukwepaji kodi: +255 22 213 7638 / +255 784 210 209

 “Pamoja Tunajenga Taifa Letu”

Post a Comment

0 Comments