HABARI MPYA YA LEO KUTOKA SIMBA NA YANGA KUELEKEA MECHI YA JUMAMOSI...MAMBO NI MOTO

WAKATI Yanga ikitamba kikosi chake kimeimarika kila idara, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco amesema kuwakosa wachezaji, Chris Mugalu na Thadeo Lwanga katika mechi ya keshokutwa kwake ni 'pigo kubwa', lakini ameahidi haitawazuia kuondoka na pointi tatu muhimu katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya NBC.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Pablo, raia wa Hispania alisema wachezaji hao walioko katika kikosi cha kwanza bado ni majeruhi, hivyo hawatakuwa sehemu ya mipango yake kuelekea mechi hiyo.


Pablo alisema alihitaji kuona wanatumia uzoefu wao wa mechi 'kubwa' ili kuongeza nguvu lakini tayari ameshapata nyota wengine ambao amewaandaa kuonyesha kiwango kizuri.


"Nimetoka kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutinga hatua ya makundi, hivyo ningehitaji siku nyingine tatu za maandalizi, lakini haiwezekani. Nakwenda kuwakosa wachezaji wangu muhimu (Thadeo Lwanga na Chris Mugalu) katika mechi hiyo, sitaki visingizio, tutapambana ili tushinde mechi hiyo, tupate pointi tatu na nina imani tutashinda, ingawa wapinzani wetu ni wazuri na wana wachezaji wazuri pia," alisema Pablo.

Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ametamba kikosi chake kiko imara katika kila idara.
Nabi alisema kila mchezaji yuko tayari kupambana ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kuendelea kujiimarisha katika msimamo wa ligi.


"Tunaendelea kujiimarisha ili tuwe imara zaidi katika kila idara, ni mechi ambayo hutakiwi kufanya makosa, Simba ina wachezaji wenye uzoefu na uwezo, hivyo tunatakiwa kutowapa nafasi, kutofanya makosa," Nabi alisema.

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema jana maandalizi ya mechi hiyo ya watani yanaendelea vizuri na shirikisho limejipanga kuhakikisha kila mmoja anatekeleza vyema majukumu yake.


Ndimbo alisema mashabiki wanatakiwa kufuata taratibu zote ikiwamo kununua tiketi mapema ili kukwepa usumbufu wa msongamano wakati wa kuingia.

“Kiutawala tuko vizuri, mamlaka husika imesimamia vizuri suala la usalama, kikubwa mashabiki wajitokeze kwa wingi na mapema ili kuepusha msongamano wakati wa kuingia getini,” alisema Ndimbo.



Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema wachezaji wao wote wako fiti ingawa wataendelea kumkosa straika, Yacouba Sogne ambaye bado yuko katika matibabu.

“Tumejiandaa vizuri, tuko tayari kwa mchezo huo, tuombe Mungu tusiwe majeruhi kwa pande zote mbili, kikubwa Yanga tumejiandaa vizuri na wachezaji wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya kwenda kutafuta matokeo mazuri na kujiimarisha zaidi kubaki kileleni,” alisema Bumbuli.

Ally Shatry (Chiko), Kaimu Ofisa Habari wa Simba, aliliambia gazeti hili kikosi chao kilichorejea nchini juzi kutoka Zambia kiliingia kambini moja kwa moja ili kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi.

“Kikosi kipo imara na kila mchezaji anautaka huu mchezo kwa sababu tunahitaji kupata pointi tatu ili kurejea katika nafasi yetu ya kuongoza ligi, hatutakuwa tayari kupoteza mara mbili dhidi ya Yanga,” alisema Chico.

Simba inakwenda kucheza mechi hiyo ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ikiwa na kumbukumbu kuchapwa bao 1-0 kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 25, mwaka huu.

Lakini itakuwa ni 'dabi' ya kwanza ya Pablo tangu ajiunge na timu hiyo mwezi uliopita, ikiwa ni mechi yake ya tano ya mashindano. Tayari ameshaiongoza Simba kwenye mechi nne, mbili za kimataifa na mbili za Ligi Kuu, akishinda mechi tatu na kupoteza moja.

Mechi mbili ni za Kombe la Shirikisho dhidi ya Red Arrows ya Zambia ya nyumbani na ugenini ikishinda mabao 3-0 nyumbani na kufungwa mabao 2-1 Lusaka, huku ikiwa imecheza mechi mbili za Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting ikishinda mabao 3-1 na Geita Gold ikishinda mabao 2-1.

Post a Comment

0 Comments