AFARIKI KWA KUGONGWA NA NDEGE YA FASTJET UWANJA WA NDEGE MWANZA

Mkazi mmoja wa mkoa wa Mwanza amefariki dunia baada ya kuigonga ndege ya Fastjet iliyokuwa ikiruka katika Uwanja wa Ndege Mwanza kuelelea jijini Dar es Salaam.

Kaimu MKurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela amesema tukio hilo la aina yake limetokea jana usiku.

Amesema ndege hiyo ilikuwa njia moja kuelekea jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa mtu huyo ndiye aliyeigonga ndege hiyo.

“Ingawa ndege ndiyo ilimgonga mtu huyo ambaye jina lake hatulifahamu, kisheria mtu au kitu chochote kinachokuwa kwenye njia ya kurukia na kutua ndege ndiyo kinahesabiwa kuigonga ndege. Ni kama ilivyo kwa treni,” amesema Mayongela.

Amesema kabla ya ndege hiyo kuruka, taratibu zote za kiusalama zilifuatwa ikiwemo kukagua njia kujiridhisha hakuna kitu chochote.

“Haijulikani mtu huyo alitokea wapi. Vyombo vya ulinzi na usalama vipo eneo la tukio kuchunguza tukio hilo kwa kina na tutatoa taarifa kamili uchunguzi utakapokamilika,” amesema kaimu mkurugenzi huyo.

Amesema kitendo cha mtu huyo kuwepo katika njia ya kurukia ndege licha ya ukaguzi kufanyika kinawaumiza vichwa viongozi na wataalam wa usalama uwanjani hapo.

“Pengine tatizo la muda mrefu la kukosa uzio tunaloanza kukabiliana nalo kwa ujenzi na upanuzi wa uwanja linaweza kuwa chanzo cha mtu huyo kuingia katika njia ya kurukia ndege,” amesema.

Ili kukabiliana na matukio ya aina hiyo, amesema wataimarisha mifumo ya usalama kwenye viwanja vya ndege nchini.
Chanzo- Mwananchi

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.