CAG AIBUA SAKATA LA LUGUMI
Sakata la mkataba baina ya Kampuni ya Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi, halijafa; ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeliibua ikionyesha madoa lukuki.
Sakata hilo lilikuwa kama limezikwa baada ya kamati iliyoundwa na Bunge kulichunguza na baadaye kukabidhi ripoti ofisi ya Spika ambayo ilisema ingeishauri Serikali cha kufanya.
Juni 30 mwaka jana, Naibu Spika Tulia Ackson alilieleza Bunge kuwa ametumia kanuni ya 117(17) kuikabidhi Serikali matokeo ya uhakiki uliofanywa na kamati ndogo iliyoundwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Alisema matokeo ya ripoti hiyo yana maoni, ushauri, mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto zilizoainishwa na taarifa ya kamati ya PAC na hivyo kuzuia wabunge kujadili suala hilo.
Lakini, ripoti ya CAG iliyotolewa wiki iliyopita imeibua upya sakata hilo, ambalo linahusu utekelezwaji mbovu wa mkataba wa uwekaji mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole (Automated Fingerprint Identification System-Afis).
Ripoti ya CAG inaonyesha kuwa Lugumi Enterprises kufunga mashine katika vituo 36 kati ya 152, hii ikiwa ni tofauti na ukaguzi wa awali ulioonyesha kuwa kampuni hiyo ilikuwa imefunga mashine hizo katika vituo 14 tu kati ya 108 ilivyotakiwa kufunga na kulipwa asilimia 99 ya malipo kwa mujibu wa mkataba.
Ripoti mpya ya CAG pia inaonyesha kuwa mamlaka husika zilisababisha mradi huo kutumia Sh41 bilioni badala ya Sh37 bilioni kama ilivyoonekana katika ukaguzi wa awali uliofanywa katika kipindi kilichoishia Juni 30, 2014.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba aliomba muda wa kufuatilia taarifa hiyo alipoulizwa na Mwananchi kuhusu ripoti hiyo mpya ya CAG.
“Subiri nifuatilie niione halafu tutawasiliana,” alisema Advera.
Sakata hilo la mkataba wa Kampuni ya Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi liliibuliwa mwanzoni mwa mwaka jana baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kubaini ufisadi katika utekelezaji wake.
Katika mkataba huo ilibainika kwamba kampuni hiyo ililipwa Sh34 bilioni sawa na asilimia 99 ya fedha zote za mradi ambazo zilikuwa Sh37 bilioni. Ilifunga mashine katika vituo 14 vya polisi mkoani Dar es Salaam.
Wabunge walimtaka aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kuwajibika kwa madai kuwa alikuwa mmoja wa wanahisa wa kampuni ya Infosys iliyoshiriki katika mradi huo.
Wakati sakata hilo likikolea Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa Kitwanga, akieleza kuwa aliingia bungeni kujibu maswali ya wizara yake akiwa amelewa.
Ripoti mpya ya CAG ya kipindi cha 2015/16 inaeleza kuwa uchunguzi uliofanywa Wizara ya Mambo ya Ndani katika ununuzi wa teknolojia ya mfumo wa kielektroniki wa uhamiaji (E- immigration System) kwa ajili ya Idara ya Uhamiaji, Lugumi Enterprises ilibabaisha katika uwasilishaji wa makabrasha ya zabuni.
Ripoti inasema kuwa Lugumi iliwasilisha makabrasha mawili tofauti ya zabuni yenye bei tofauti ya Sh37.1 bilioni na 39.5 bilioni, jambo lililoathiri uthibitisho wa kabrasha sahihi.
Pia kamati ya tathmini ilishindwa kubaini makosa yaliyowasilishwa na Lugumi, hali iliyosababisha bodi ya zabuni kuidhinisha bei ambayo haikuwa halisi hivyo kusababisha mabadiliko ya gharama za mkataba kutoka Sh37 bilioni kwenda Sh41 bilioni.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba, wajumbe wawili wa kamati ya tathmini hawakutia saini ripoti ya tathmini wala kujaza fomu za agano kinyume na Kifungu cha 37(6) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma (PPRA) ya mwaka 2011.
Maeneo mengine yaliyotajwa ni pamoja na mkataba wa Lugumi na wizara kuonekana kuwa na baadhi ya vitu vyenye mchanganuo sawa, lakini bei zake zikiwa tofauti, hali iliyosababisha hasara ya Sh656.7 milioni.
Pia, kuna Sh1 bilioni zilizolipwa kama gharama ya mafunzo, lakini mafunzo hayo hayakufanyika wakati Sh3 bilioni zililipwa kwa ajili ya matengenezo lakini pia hayakufanyika.
Pia Lugumi imeonekana kutolipa kodi.
“Hapakuwa na uthibitisho kuwa mzabuni alilipa kodi kwa TRA yenye thamani ya Sh2.2 bilioni kati ya Sh5.7bilioni zilizopaswa kulipwa licha ya mzabuni kupata msamaha wa kodi wa Sh3.5 bilioni katika mkataba wa Sh37 bilioni,” inasema ripoti hiyo.
Pia inaonyesha kuwa baadhi ya gharama za vifaa katika mkataba zilikuwa juu kulinganisha na bei ya soko na hivyo kusababisha hasara ya Sh5.9 bilioni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ililiagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wakala wa Tehama (e-GA) wa Serikali kufanya tathmini ya kina ya mfumo huu ili kutoa mapendekezo ya hatua madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya vifaa vilivyofungwa.
Pia iliagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) ifanye tathmini ya kina kama mzabuni alilipa kodi zote zinazostahili katika mkataba, mamlaka za nidhamu zichukue hatua kwa mkuu wa idara ya ununuzi kwa kuidhinisha makabrasha ya zabuni yasiyokuwa sahihi, wajumbe wa kamati ya tathmini kwa kushindwa kubaini makosa katika zabuni.
Pia ilishauri kuchukuliwa hatua kwa maofisa waliohusika katika mapokezi ya vifaa kwa kukubali kuvipokea wakati havikidhi masharti ya mkataba.
Wengine wanaostahili kuchukuliwa hatua ni wajumbe wa Bodi ya Zabuni waliohusika kuidhinisha zabuni kwa Lugumi wakati wakijua hakustahili.
Akizungumzia sakata hilo na ripoti ya CAG, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Fordia, Bubelwa Kaiza alisema ripoti hiyo imeweka wazi ukweli wote, hivyo sheria ichukue mkondo wake.
Pia, alishauri PPRA kwa kutumia mamlaka yake ifute zabuni ya Afis kwa kampuni hiyo ya Lugumi.
Akizungumzia ripoti ya CAG, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema hotuba ya maoni ya kambi ya upinzani imejaa taarifa nyingi zaidi kuhusu zabuni na mkataba huo na madudu mengine.
Alisema tayari anazo taarifa za kutosha zenye ushahidi kuhusu sakata hilo kwa kuwa anataka kumsaidia Rais Magufuli kufahamu asiyoyafahamu na kuchukua hatua.
“Hotuba yangu itakuwa na ukali wenye lengo la kuibua udhaifu huo. Itakuwa imeainisha wazi zaidi sakata hilo, itakuwa ya tofauti na nisingependa kueleza kwa kina kuhusu hotuba ila kwa ufupi hakuna jiwe litakalobakia juu ya jiwe safari hii,” alisema Lema.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi