Monday, January 27 2025

Tundu Lissu ahojiwa polisi kwa saa sita



MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) jana alihojiwa na Polisi jijini Dar es Salaam kwa saa sita, kuhusu mkutano wake na wanahabari wiki iliyopita kuzungumzia kupotea kwa Ben Saanane.

Saanane ni Mkuu wa Idara ya Utafiti na Sera wa Chadema na msaidizi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na ilielezwa alipotea tangu Novemba 14 mwaka huu na mpaka sasa haijajulikani alipo.

Akizungumza jana, Lissu alisema hakukamatwa, bali aliitwa kuhojiwa kuhusu mkutano wake na wanahabari wiki iliyopita.

“Sijakamatwa ila nimeitwa kuhojiwa kuhusu ile ‘Press Conference’ (mkutano na waandishi wa habari) ya wiki iliyopita na nimetakiwa nitoe maelezo kuhusu Saanane. “Nilitakiwa nifike polisi saa mbili asubuhi kituo cha kati (kituo kikuu). Nimefika saa nne kuhojiwa kuhusu mambo mawili; moja nitoe ushahidi kuhusu kupotea kwa Ben Saanane na kauli zilizoitwa za uchochezi nilizozitoa katika mkutano wangu na waandishi wa habari,” alisema Lissu aliyehojiwa hadi saa kumi jioni.

Hivi karibuni, Lissu alisema Chadema haifahamu alipo Saanane na kuitaka serikali ieleze mahali alipo msaidizi huyo wa Mbowe kwa kuwa moja ya kazi za chombo hicho ni kulinda raia wake.

Hata hivyo, juzi Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Boaz, alisema Polisi haijui alipo Saanane na inaendelea na uchunguzi wa kina kubaini alipo kiongozi huyo wa Chadema.

Aidha, alieleza kuendelea na uchunguzi wa miili saba iliyokutwa kando ya Mto Ruvu wilayani Bagamoyo ikiwa imefungwa katika mifuko ya sarandusi.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.