Mwandishi wa ITV Halfan Lihundi aachiwa huru
Mwandishi wa kujitegemea wa kituo cha televisheni cha ITV, Halfani Lihundi ameachiwa kwa dhamana kutoka katika kituo cha Polisi cha Changamoto, Usa River wilayani Arumeru mkoani Arusha alikokuwa anashikiliwa tangu juzi, na kutakiwa kuripoti kituoni hapo Desemba 27, mwaka huu.
Alikuwa anashikiliwa kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, baada ya kuripoti habari inayoelezwa na mkuu huyo wa wilaya kuwa haikuwa sawa na kuamuru kukamatwa kisha, kulala mahabusu na hatimaye kufanikiwa kutoka jana saa tisa alasiri.
Awali, waandishi wa habari wa Arusha walikusanyika kituoni hapo ili kujua hatma ya mwenzao na baadaye kuamua kwenda kumuona Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ili kumweleza kuwa mwenzao amekamatwa kwa sababu ya migogoro ya wananchi.
Wakati Lukuvi anatoka kwenye kikao cha kujadili migogoro ya ardhi kilichofanyika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, waandishi waliimba wimbo wenye lengo la kufikisha ujumbe kuwa, wanataka wenzao aachiwe huru. Waliimba; “Solidarity Forever, Bring Back Halfani Lihundi.”
Lukuvi alisema hahusiki na suala hilo na kuwasihi wanahabari kwenda naye Usa River kwenye mkutano ambapo Mnyeti atatoa tamko juu ya suala hilo.
Lakini Mnyeti alipokuwa akitoka kikaoni hapo aliulizwa na waandishi kuhusu suala hilo na kosa lipi limefanya Lihundi kushikiliwa Polisi, lakini hakuzungumza chochote na kuelekea kwenye gari lake kusubiri msafara wa Lukuvi.
Awali, ilidaiwa kuwa Mnyeti ndiye aliyeamuru Lihundi akamatwe kwa madai ya kuandika habari za uchochezi za kijiji cha Leguruki, Arumeru.
Alisema alipotaka kujua kosa analoshitakiwa nalo Lihundi, alijibiwa hana kosa ila yupo kwa amri ya Mkuu wa Wilaya. Hata hivyo, RB ya Polisi Usa River 4763/2016 inaonesha ana kosa la uchochezi.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi